Kocha riadha azivuruga BMT, RT

Muktasari:

Kocha huyo aliyekuja nchini kutokana na ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo Japan (JICA) na Tanzania, anatarajiwa kuanza kazi Novemba 27. Naibu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alisema, Sato atakuwepo nchini hadi mwaka 2020. Sato alisema anataka kuipa mafanikio Tanzania.

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kumtangaza Ayne Sato kuwa kocha wa mchezo huo nchini, Katibu Mkuu Wilhelm Gidabuday amesema Mjapan huyo amekuja nchini kufanya kazi za kujitolea.

Gidabuday alisema Ron Davis, raia wa Marekani ndiye kocha mkuu wa riadha na alipitishwa na Kamati ya Utendaji ya RT.

Gidabuday alisema, Davis aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa iliyoshinda medali mbili za fedha katika Olimpiki ya mwaka 1980 ndiye kocha mkuu na Sato atafanya majukumu mengine ambayo atapangiwa na RT.

Alisema Sato amekuja kufanya kazi kwa kujitolea na RT haitamlipa mshahara, lakini Davis ni mwajiriwa wa shirikisho hilo na atalipwa mshahara.

Awali, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na RT walimtambulisha Sato kuwa kocha wa riadha atakayefundisha mbio fupi (mita 100, 200, 400), kati (mita 800 na 1500) na miruko.