Kocha mpya Yanga kutua na mastraika wawili,Yondani aanza kuaga

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumamosi wakati akipata lanchi yake, Maxime aliweka wazi kwamba hata uongozi wake wa Kagera unajua kuwa msimu ujao anakwenda Yanga

KOCHA wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesisitiza kwamba kila kitu chake na Yanga kiko sawa na sasa ni suala la muda tu atue Jangwani rasmi kama Kocha msaidizi wa Luc Eymael msimu ujao.

Lakini akasisitiza kwamba kuna uhitaji wa kupatikana mastraika wawili wapya mafundi zaidi ya Mkongomani Heritier Makambo aliyeuzwa na Yanga.

Maxime ni miongoni mwa makocha wazalendo waliocheza mpira kwa mafanikio na kustaafu kwa heshima ndani ya Taifa Stars bila kucheza Simba wala Yanga.

Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumamosi wakati akipata lanchi yake, Maxime aliweka wazi kwamba hata uongozi wake wa Kagera unajua kuwa msimu ujao anakwenda Yanga.

Kocha huyo aliyekuwa akicheza nafasi ya beki enzi zake, alisema katika kutua kwake Yanga atapendekeza zisajiliwe mashine mbili za maana na angefurahi zaidi kama moja wapo ikiwa Heritier Makambo wa AC Horoya wa Guinea. Lakini Mwanaspoti linajua Yanga wamejaribu kwenye siku za karibuni kumshawishi Makambo lakini tatizo ikawa ni gharama za mkataba wa Horoya.

“Yule Makambo kama watampata ni mtu hasa anayelijua goli,Yanga haina mtu wa namna hiyo kabisa kwasasa, kama unakuwa na viungo kama ambao wapo sasa pale akija yule kwa kasi yake ya mabao ya mguuni na hata shabaha ya kichwa chake hakuna atakayetoka salama,”alieleza Maxime ambaye amezichachafya Simba na Yanga akiwa na vikosi vya Kagera na Mtibwa kwa misimu tofauti tena vikiwa vimesajili kwa bajeti za wastani.

“Hakuna mfungaji pale kwasasa ndio maana unaona timu inasumbuka sana,nafikiri mtu kama Makambo atarudisha uhai yule sio mshambuliaji wa kupata nafasi tatu akapoteza zote,”aliongeza.

Mbali na Makambo Maxime alisema Yanga kama watamkosa Mkongomani huyo basi atashauri wamuangalie hata Mzambia Obrey Chirwa ambaye bado kwake ni mshambuliaji mzuri.

“Hata yule Chirwa anajua sana watu wanamuona kama kamaliza lakini anaijua kazi yake, uzuri wa hawa sio wageni wa maisha ya Yanga kuanzia uchezaji mpaka maisha ya ndani kwahiyo hawahitaji sijui kuzoea,”alisema huku akisisitiza kuwa bado hajajua Yanga watakuwa wamejipangaje mpaka msimu utakapomalizika aingie ndani aone rasmi mambo yatakuwaje na mawazo ya Eymael yakoje.

Maxime anaamini kwamba kwa nafasi yoyote ile ambayo Yanga watamaliza msimu huu, wakipata mastraika wapya wawili pamoja na marekebisho mengi ya kimsingi watakayojadili kama benchi la ufundi anaamini kwamba Yanga mpya yenye raha zaidi inakuja.

“Mimi kuwa Kagera mpaka sasa ni heshima tu Yanga walishakamilisha karibu kila kitu kuhusu kwenda kwao unajua hili ni suala la muda mrefu sana,”alisema Maxime.

“Kagera waliniomba kwa wakati ambao Yanga walinihitaji wasingeweza kumpata mtu wa kuchukua nafasi yangu na ingewezekana wangesumbuka kidogo kwenye ligi wakaniomba mimi pamoja na Yanga nimalize msimu.

“Nafikiri msimu kama utamalizika sasa kuna mambo yataendelea ni huu ugonjwa wa corona tu unachelewesha mambo sina wasiwasi katika kufanya kazi yangu,”aliongeza Kocha huyo ambaye timu yake iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi yenye timu 20 na hana nafasi ya kubeba ubingwa msimu huu.

YONDANI AAGA

Mikataba inayozungumzwa sana ni ile Papy Tshishimbi, Bernad Morrison lakini hata beki mkongwe Kelvin Yondani mkataba wake unamalizika lakini cha ajabu ni kwamba viongozi wamemchunia.

Uchunguzi wa Mwanaspoti ndani ya Yanga umebaini kwamba viongozi hao hawajapewa maelekezo yoyote na Kocha Luc Eymael kuhusiana na Yondani ambae amekuwa hampangi licha ya kuwa kipenzi cha mashabiki. Lakini mmoja wa mastaa wa Yanga aliiambia Mwanaspoti kwamba Yondani ambae amezima simu zake zote na kujichimbia gheto kwake Kigamboni, amewajulisha baadhi ya wachezaji marafiki zake ndani ya Yanga kwamba anarudi Simba.

Mmoja wa mastaa wa Yanga aliidokeza Mwanaspoti kwamba Yondani amewaambia wachezaji watatu wa safu ya ulinzi kuwa haoni mwanga wa maisha yake tena ndani ya timu hiyo na kwamba suluhisho pekee anaona ni kurudi Msimbazi ambako wamekuwa wakimsaka muda mrefu.

Viongozi wa Yanga jana hawakutoa ushirikiano kuhusiana na ishu ya Yondani ingawa inavyoonekana bado faili lake lipo mbali kujadiliwa.

3-0

Yanga ilifungwa mabao 3-0 na Kagera katika mechi ya Ligi msimu huu ndani ya Uwanja wa Taifa. Marudiano ni hivikaribuni mjini Bukoba.