Kocha mpya KMC siri nzito

Muktasari:

Ndayiragije amejiunga na Azam FC kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuiongoza KMC kumaliza kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu msimu ulioisha pamoja na kufika nusu fainali ya Kombe la FA.

WAKATI  KMC ikimuongezea mkataba wa miaka mitatu mshambuliaji wake Charles Ilanfya, uongozi wa klabu hiyo umefichua mipango ya kimyakimya ya kumsaka kocha mkuu mpya atakayerithi mikoba iliyoachwa na Etienne Ndayiragije aliyetimkia Azam FC.
Ilanfya aliyesaini mkataba huo juzi jijini, anakuwa mchezaji wa tatu kufanya hivyo akifuata nyayo za Ally Ally na Hassan Kabunda ambao nao wamemwaga wino wa kuendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Hata hivyo, wakati kasi ya kuendelea kuongeza mikataba ya nyota wake waliomo kikosini ikiendelea, timu hiyo imesisitiza kuwa bado inaendelea na mchakato wa kumsaka kocha mkuu mpya ambao wanaufanya kwa usiri mkubwa.
"Ni jambo la kawaida kwamba pindi kocha mkuu anapoondoka kujiunga na timu nyingine, pengo lake linatakiwa kuzibwa hivyo kwa upande wetu KMC tayari tumeanza mchakato wa kumsaka kocha mpya na idadi kubwa ya makocha kutoka ndani na nje ya nchi wametuma wasifu na maombi ya kuifundisha timu yetu.
"Hata hivyo kutokana na uzito wa jambo lenyewe, hatuwezi kutaja hata majina ya hao walioomba hadi pale ambapo klabu itakapomtangaza rasmi lakini niwadokeze tu kwamba uongozi uko makini na tutampata kocha bora ambaye kila mdau wa soka nchini hatoamini," alisema Ofisa Habari wa KMC, Anwar Binde.
Binde anasema uongozi wa KMC unafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara msimu ujao ambao watakuwa na jukumu zito la kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA.
Ikumbukwe kwamba kwa sasa KMC haina kocha mkuu baada ya kuachana na Nadyiragije ambaye amejiunga na Azam kwa mataba wa miaka miwili.