Kocha mpya Harambee Stars, zake ni chocha tu

Muktasari:

Tayari mipango yake ni kuhakikisha Stars inafuzu kwa dimba la AFCON 2021.

BAADA ya kutambulishwa rasmi  hivi majuzi kama Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Soka Harambee Stars, Mkufunzi, Francis Kimanzi kachocha kinoma.

Ikiwa ni mara yake ya tatu kuteuliwa kwenye wadhifa huo, kocha huyo kadai safari hii  anakuja na ubaya sana.

Kimanzi kadai kuwa tajriba na ukufunzi atakaouleta kwenye timu safari hii, utakuwa wa kiwango cha juu ikilinganishwa na vipindi vyake vya hapo awali alipokalia wadhifa huo.

“Laiti ningelikuwa na ufahamu na uzoefu nilionao sasa hivi miaka kumi iliyopita, basi naamini tungelifanya vizuri zaidi ya tulivyo sasa.

“Narejea na uzoefu usiokuwa wa kawaida na ufahamu mpevu zaidi wa kisoka tofauti na vipindi vyangu vya awali nilipokuwa hapa. Nyie wenyewe mtakuwa mashahidi,” Kimanzi kachocha.

Tayari mipango yake ni kuhakikisha Stars inafuzu kwa dimba la AFCON 2021.

“Nafikiri itakuwa jambo nzuri zaidi kwetu kuhakikisha tunafuzu tena kwa dimba la AFCON kabla ya kuanza kuwazia mashindano mengine kama vile Kombe la Dunia,” aliongeza.

Stars imepangwa kwenye kundi moja na Misri, Comoros na Togo kwenye mechi za kufuzu ushiriki wa AFCON 2021.

Stars ilishiriki katika makala ya mwaka huu ya dimba hilo la AFCON kule Misri na kuishia kufanya vibaya sana.

Stars pia imetolewa kwenye michuano ya Chan kwa wachezaji wanaocheza klabu za nyumbani na ilitupwa nje na Taifa Stars ya Tanzania kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare kwenye michezo yote miwili, ule wa Tanzania na marudiano uliopigwa nchini.

Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kurejea katika dimba hilo baada ya miaka 15.  Sasa Kimanzi kaahidi kuhakikisha Stars inafuzu kwenye mkondo ujao.

Japo wapo wadadisi waliotilia shaka uteuzi wake kwenye kwa mara ya tatu, Kimanzi anakumbukwa kwa mafanikio kadhaa aliyoweza kuzalisha alipokuwa na timu hiyo hapo nyuma.

Mpaka leo, Kimanzi ndiye kocha wa pekee aliyefanikisha Stars kuishia kuorodheshwa katika nafasi yake bora zaidi duniani na FIFA ilipokamata nafasi ya 68, 2008, mwaka ambao pia alitwaa taji la Ligi Kuu na klabu ya Mathare United.

Alifutwa Januari 2009 kabla ya kuteuliwa tena Novemba 2011.

Kimanzi kasaini mkataba wa miaka miwili na Shirikisho la soka nchini FKF.