Kocha mpya Man United shida tupu

Muktasari:

  • Makocha wanaotajwa kwenye kibarua hicho cha Old Trafford ni Laurent Blanc, Zinedine Zidane, Mauricio Pochettino, Marco Rose, Diego Simeone, Southgate na Solskjaer mwenyewe.

MANCHESTER, ENGLAND . UNAAMBIWA hivi, kama kuna kipindi kigumu zaidi kilichowahi kuwakabili Manchester United katika uteuzi wa kocha mpya tangu alipoondoka Sir, Alex Ferguson basi ni kipindi hiki cha sasa cha kuelekea mwisho wa msimu.

Kocha, Jose Mourinho ameondoka kwenye kikosi hicho mwezi uliopita na kuacha nafasi wazi inayopaswa kuzibwa. Kwa sasa kikosi hicho, kipo chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer, ambaye kwenye mechi sita alizoisimamia timu hiyo hadi sasa, Man United imeshinda zote.

Makocha wengi wanahusishwa na kibarua na sasa jina jipya lililotajwa hivi karibuni ni la Gareth Southgate, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya England.

Makocha wanaotajwa kwenye kibarua hicho cha Old Trafford ni Laurent Blanc, Zinedine Zidane, Mauricio Pochettino, Marco Rose, Diego Simeone, Southgate na Solskjaer mwenyewe.

Bosi wa Man United, anayehusika kwenye uteuzi huo wa kocha mpya, Ed Woodward atakuwa na kazi kubwa ya kupitia rekodi ya kila kocha na kuona kama kuna uwezekano wa kupewa kibarua hicho kigumu kilichowashinda David Moyes, Louis van Gaal na Mourinho.

Takwimu zipo hivi. Kwenye rekodi zake za ukocha, Blanc ameshinda mechi 234, sare 66 na vichapo 56. Mataji aliyobeba, Ligue 1 mara nne, Kombe la Ugaransa mara mbili, Kombe la Ligi mara nne na French Super Cup mara tano.

Pochettino rekodi yake inasomeka kwamba, ameshinda mechi 219, sare 53 na amepoteza mechi 54, huku akiwa hajawahi kushinda taji lolote wenye maisha yake, lakini kubwa ni uzoefu wake kwenye Ligi Kuu England, akizinoa timu za Southampton na Tottenham na kufanya vizuri licha ya kuwa na bajeti ndogo katika kufanya usajili.

Kocha, Marco Rose yeye ameshinda mechi 134, sare 47 na amefungwa mara 24. Taji kubwa alilowahi kubeba ni la ubingwa wa Ligi Kuu huko Austria, Austrian Bundesliga mara moja. Aliwahi kuifikicha pia klabu ya Salzburg kwenye nusu fainali ya Europa League.

Simeone, ameshinda taji la Ligi Kuu Argentina mara mbili, La Liga mara moja, Kombe la Hispania mara moja, Spanish Super Cup mara moja, Europa League mara mbili na Uefa Super Cup mara mbili pia. Kocha huyo Muargentina amekuwa akifanya vizuri kwelikweli huko kwenye kikosi cha Atletico Madrid na kama Man United itamchukua basi huenda wakawa na wepesi wa kumchukua, Antoine Griezmann kwenye kikosi chao huko Old Trafford.

Solskjaer, ambaye kwa sasa ameshika kibarua hicho kwa muda, rekodi zake ni kwamba ameshinda mechi 149, sare 49 na amechapwa kwenye mechi 80 katika kibarua chake cha ukocha. Mataji aliyowahi kubeba ni Ligi Kuu Norway mara mbili na Kombe la Norway mara moja.

Solskjaer ana miezi sita ya kuwashawishi mabosi wa Man United kumpa kibarua hicho cha kudumu, ambapo kwa sasa kwenye mechi sita alizocheza, ameshinda zote.

Kuhusu Southgate ni kwamba yeye ameshinda mechi 89, ametoka sare mara 54 na amefungwa mara 72. Hajawahi kushinda taji lolote, jambo hilo linamfanya kujiweka kwenye nafasi finyu sana ya kuchaguliwa kuwa kocha wa wababe hao wa Manchester.

Zidane aliachia ngazi Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita. Rekodi zake kwenye ukocha ni kwamba ameshinda mara 130, sare 46 na kupoteza mara 30. Mataji makubwa aliyobeba ni pamoja na La Liga mara moja, Spanish Super Cup mara moja, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, Uefa Super Cup mara mbili na Klabu Bingwa Dunia mara mbili. Zidane ni kocha aliyeonyesha kuwa na uwezo mkubwa kwa muda wake aliokuwa kwenye kikosi cha Los Blancos, lakini shida yake kubwa ni kwamba si mzuri kwenye kufanya usajili, lakini kama atakamatia kibarua cha Old Trafford anaweza kuwababe Cristiano Ronaldo, Luke Modric na Sergio Ramos kuja kumfanyia kazi yake kwenye Ligi Kuu England.