Kocha aukubali mziki wa Chilunda

Monday December 10 2018

 

By Eliya Solomon

LICHA ya lugha gongana, Kocha wa CD Tenerife, Mhispania, José Luis Oltra amemkingia kifua mshambuliaji wake wa Kitanzania, Shaaban Idd Chilunda kuwa atakaa sawa kutokana na kukumbana na changamoto ya mawasiliano.

Tangu alipojiunga na CD Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania, akitokea Azam FC, Agosti mwaka huu, Chilunda amekuwa kwenye wakati mgumu kutona na lugha inayotumika kimawasiliano ndani ya klabu hiyo kuwa ni Kihispania.

Hivi karibuni kwenye moja ya mahojiano yake, Oltra alisema anatambua uwezo wa mshambuliaji huyo lakini bado yupo kwenye mazingira magumu ya mawasiliano.

“Shida kwa Chilunda ni kwenye lugha tu. Ni ngumu kuelewa baadhi ya mambo kwa wepesi kutokana na changamoto hiyo ambayo anakabiliana nayo, yuko vizuri uwanjani na naamini atakaa sawa,” alisema kocha huyo.

Upande wake Chilunda mwenye umri wa miaka 20, aliwahi kukiri kuwa kwenye changamoto hiyo wiki kadhaa nyuma alipokuwa nchini kwa majukumu ya kulitumikia taifa.

“Bado sijakaa sawa kwenye inshu ya mawasiliano kwa hiyo ni ngumu hata kwenda saluni na kusema nataka kuonyolewa kwa staili fulani,” alisema Chilunda na kucheka.

Wakati huo Chilunda alipokuwa akizungumza na Mwanaspoti alikuwa akinyolewa na mchezaji mwenzake kwenye kambi ya Taifa Stars ilikuwa ikijiandaa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani.

Advertisement