Kocha amshtua Kagere Simba

Sunday July 5 2020

 

By ELIYA SOLOMON

KOCHA wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ ametamka maneno ambayo straika wa Simba, Meddie Kagere akiyasikia huenda yakamshtua; “Ningependa watu wabaki na maneno yangu, kama Kagere asipozinduka inakula kwake.”

Anasema mchezaji huyo atapinduliwa katika vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu.

Kagere anaongoza orodha ya wafumania nyavu wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 19 huku akifuatiwa na Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar mwenye mabao 13 na Reliants Lusajo kabla ya mchezo ya jana.

Bares, ambaye jana alikuwa akikiongoza kikosi chake cha JKT Tanzania kucheza dhidi ya Namungo, alisema kama Mhilu na Lusajo wakiongeza kasi wanaweza kumpindua Kagere mwenye umri wa miaka 33.

“Mpira umekuwa na mambo mengi ya kushangaza, ningependa watu wabaki na maneno yangu, kama Kagere asipozinduka kwa sababu kwa sasa ni kama yupo usingizini basi huenda akazidiwa kwa mabao na wakina Mhilu na wenzake.

“Kwanza kwa sasa amekuwa akianzia benchi na badala yake tumekuwa tukiona akicheza Bocco hivyo lolote linaweza kutokea katika michezo iliyobaki kabla ya msimu kumalizika,” alisema kocha huyo wa zamani wa Tanzania Prisons.

Advertisement

Upande wake, Mhilu ambaye jana alikuwa na mchezo wa Ligi ambapo walikuwa wakicheza dhidi ya Ruvu Shooting anaamini kwa michezo iliyobaki anaweza kufikia malengo yake ya kufunga mabao 20 ndani ya msimu huu.

“Ikitokea nimekuwa mfungaji bora litakuwa jambo jema ila malengo yangu ya msimu huu ni kufunga mabao 20, nimebakisha hatua chache ambazo naamini nitazimaliza,” alisema.

Msimu uliopita Kagere alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kupachika mabao 23 ambayo yaliisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi hiyo kwa mara pili mfululizo.

Advertisement