Kocha afichua ishu ya Carlinhos Yanga

KOCHA wa Yanga, Zlatko Krmpotic amesema Carlos Fernandez ‘Carlinhos’ bado hayupo fiti kukipiga dakika 90, badala yake atakuwa akimtumia muda mchache.

Krmpotic alisema Carlinhos ni mchezaji mzuri mwenye kipaji lakini si muda wake wa kucheza mechi dakika zote haswa katika mechi za aina ya Tanzania Prisons.

“Wapinzani walikuwa wazuri kwenye nguvu kama timu na hata mchezaji mmoja mmoja, Carlinhos maandalizi yake hayakuwa ya kutosha kucheza mechi ya aina hii (Prisons) yenye matumizi makubwa ya nguvu kwani ilitaka mchezaji aliye fiti zaidi,” alisema.

“Nitaendelea kumuandaa Carlinhos aweze kuwa fiti na kutumika zaidi katika michezo ijayo atakapokuwa tayari kwani ni mchezaji mwenye kipaji.

TONOMBE, TUISILA

Wachezaji wawili raia wa DR Congo, Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda hawakuwa katika mipango ya kocha wa Yanga, Krmpotic kutokana na vibali vyao kuchelewa.

“Ilinilazimu kukaa nao Mukoko na Kisinda saa 10:00 jioni ili kuwaelekeza mfumo ambao tutakwenda kuutumia katika mechi hiyo,” alisema Krmpotic.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, dhidi ya Tanzania Prisons alitumia mifumo miwili alianza na 4-2-3-1, baadaye akabadilisha kwenda 4-2-4.

“Tulianza vibaya katika kipindi cha kwanza jambo ambalo natakiwa kukaa zaidi na wachezaji wangu kufanya mazoezi mengi zaidi ya kujiandaa ili kuja kufanya vizuri,” alisema.

“Wachezaji wangu wengi ndani ya timu wapo chini wanatakiwa kutambua hili ili kulifanyia kazi na tuweze kupata matokeo mazuri katika mechi nyingine za mbele zaidi,” alisema.

WACHEZAJI WAZAWA

Katika mechi na Prisons, Yanga walianza na wachezaji tisa wazawa huku wageni pekee wakiwa ni kipa Farouk Shikhalo na Michael Surpong.

Krmpotic alisema; “Wachezaji wengi hawapo tayari katika kikosi changu hawapo fiti kucheza dakika 90, haswa hawa kutoka Tanzania ila tumejipanga ili kujiandaa na kufanya vizuri baada ya kuliona hilo.”

“Wachezaji wa kigeni katika kikosi chetu wengi wao wamechelewa kufika katika maandalizi ya msimu huu jambo ambalo limenifanya kutumia wazawa wengi na hili ni tatizo kubwa lanaloweza kutokea katika mpira,” alisema kocha huyo raia wa Serbia.