Kocha Yanga akata tamaa

Muktasari:

Kocha huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha timu haishuki daraja amejipanga kuimarisha eneo la ulinzi pekee katika dirisha dogo la usajili.

Dodoma. Baada ya timu yake kupokea kichapo kingine cha mabao 4-1 wiki hii dhidi ya Baobab Queens ya Dodoma,Kocha wa Yanga Princess, Hamiss Kinonda amekubali timu yake haina ujanja.
Akifafanua zaidi Kinonda alisema mipango waliyokuwa nayo kabla ya kuanza kwa ligi imeshavurugika na sasa wanajipanga kuhakikisha timu haishuki daraja.
"Matokeo tunayoyapata yanasikitisha na hatukujipanga kufanya vibaya zaidi ya kuwa mabingwa ila kwa hali ilivyo haitawezekana zaidi ya kuhakikisha hatushuki daraja".Amesema Kinonda
Kocha huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha timu haishuki daraja amejipanga kuimarisha eneo la ulinzi pekee katika dirisha dogo la usajili.
"Licha ya ugeni wetu ila eneo la ulinzi linatuangusha zaidi na ili kuepuka kushuka nimejipanga kusajili mabeki tu katika dirisha dogo la usajili".Ameongeza kocha huyo
Kocha wa Baobab Queens,Mussa Furutuni amefurahishwa na ushindi huo ambao ameupata katika mchezo wake wa kwanza baada ya kukabidhiwa timu mwanzoni mwa wiki hii.
"Binafsi nimefurahishwa na ushindi huu kutokana na ukweli ndo nimekabidhiwa timu na mchezo wa kwanza nimeanza kwa ushindi".Amesema Furutuni
Katika mchezo huo uliochezwa uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma,mabao ya wenyeji yamefungwa na Hawa Azizi,Anastazia Joseph na Noela Patrick.