Kocha Toto Africans alia na washambuliaji wake

Friday May 22 2020

By MASOUD MASASI,MWANZA

KOCHA Msaidizi wa Toto Africans,Ally Mrisho‘Madonso’amesema wanatakapoingia kambini kuanzia Juni Mosi watajikita zaidi kukiweka sawa kikosi chao hasa safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa butu kwenye ligi Daraja la pili.

Hadi sasa Toto Africans wako katika nafasi ya tano kwenye kundi B huku  wakiwa na pointi 12 katika msimamo huo unaongozwa na wababe Kitayosce wenye pointi 24 ambao tayari wameshafuzu hatua ya Sita bora.

Akizungumza na Mwanaspoti,Madonso alisema wanahitaji kupambana na kukiweka sawa kikosi chao pindi watakapoingia kambini kwani wamebakiza mchezo mmoja na Kasulu Red Stars ambao wanahitaji sana kupata pointi tatu.

Alisema safu yao ya ushambuliaji imekuwa ikikosa umakini jambo ambalo limewafanya washindwe kufanya vyema msimu huu kitu ambacho amesema watakifanyia kazi ili mchezo huo wa mwisho waweze kupata pointi tatu.

“Tuna shida kubwa kwa washambuliaji wetu mechi tisa tulizocheza tumefunga mabao nane pekee , tutakachokifanya sasa ni kuhakikisha tunakomaa nao mazoezini ili kuwaweka sawa kwani huo mchezo na Kasulu kama tukipoteza basi tutakuwa tumeshuka daraja msimu ujao,” alisema Madonso.

Alisema wakati ligi imesimama waliwapa programu maalumu wachezaji wao ya kufanya wakiwa nyumbani haswa kutengeneza zaidi stamina hivyo watakaporejea kambini watajikita zaidi na safu hiyo ambayo wameona ndio tatizo katika kikosi chao.

Advertisement

“Hatuna shida sana katika safu ya ulinzi na kiungo tunachokifanya ni kuwapa maelekezo madogo tu kwani kazi kubwa ipo kwa washambuliaji wetu,” alisema kocha huyo ambayo alishawahi kukipiga katika klabu za 82 Rangers na Kagera Sugar.

Advertisement