Kocha Toto Africans aachia ngazi, afunguka

Thursday January 10 2019

By Saddam Sadick

Mwanza . KOCHA wa Toto Africans, Ibrahim Mlumba ametangaza kuachia ngazi katika kikosi hicho akidai kuingiliwa majukumu na kutothaminiwa na Katibu Mkuu, Chassa Yahya aliyeteuliwa kwa muda.

Mlumba ameisaidia timu kushika nafasi ya pili ikiwa pointi 11 katika Ligi Daraja la Pili katika Kundi B linaloongozwa na Gipco FC yenye alama 12.

Toto Africans iliyowahi kutesa Ligi Kuu kwa sasa haina uongozi kwani aliyekuwa mwenyekiti wake, Godwine Aiko alitangaza kujiuzuru na sasa inaendeshwa kiaina tu.

Kocha Mlumba alisema licha ya kujituma na kuwahamasisha wachezaji kucheza bila kufikiria mazingira magumu waliyonayo, lakini amekuwa akiingiliwa majukumu yake na hathaminiwi na katibu wake.

Alisema kutokana na hali hiyo hataweza kuendelea kuifundisha timu hiyo na tayari ameshapata taarifa kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kuandaliwa barua ya kusimamishwa.

“Sasa katibu anaingiliaje mazoezi ya timu badala ya kutafuta vyanzo vya pesa ili kukidhi mahitaji ya timu? Mimi sitaweza kuendelea kwa sababu naingiliwa majukumu yangu na siheshimiwi, ” alisema Kocha Mlumba.

Kwa upande wake katibu huyo wa muda Yahya, alikanusha vikali tuhuma hizo na bado anaamini Mlumba ndiye kocha wao isipokuwa anashangaa kwanini haudhurii mazoezini.

Alisema hata hivyo bado hawajajua sababu ya kocha huyo kutokuja mazoezini na iwapo ataona dalili za kuachana na timu basi watafanya haraka kusaka mbadala wake.

“Hata leo (juzi) Mlumba hajaja mazoezini na sijui tatizo ni nini kwa sababu hatudai. Bado ninaamini ni kocha wetu lakini tukiona dalili zozote za kutuachia timu, basi tutatafuta kocha mwingine wa kuziba nafasi yake”alisema katibu huyo.

Advertisement