Kocha : Simbu haendi Japan!

Muktasari:

  • Hata hivyo, kocha Francis amesema, mwanariadha huyo hatoshiriki mbio zozote hivi karibuni hadi watakapojiridhisha amepoma na hana tena maumivu ya misuli ya paja yaliyomkwamisha kwenye mbio za New York City Marathoni mwaka mwishoni mwa mwaka jana nchini Marekani ambako aliishia njiani.

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) linaamini mshindi wa medali ya shaba ya dunia, Alphonce Simbu atakwendakwenye mbio nchini Japan kusaka viwango vya kufuzu kushiriki mbio hizo msimu huu, lakini kocha wake, Francis John amesisitiza nyota huyo haendi Japan.

Francis ni kocha wa muda mrefu wa mwanariadha huyo ambaye amesisitiza kuwa, Simbu atakwenda kwenye mbio za viwango, lakini si Japan kama ambavyo RT inasema.

Juzi Jumamosi Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema wana taarifa za Simbu kwenda Japan kwenye mbio za kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika baadae Septemba mwaka huu Nchini Qatar.

Hata hivyo, kocha Francis amesema, mwanariadha huyo hatoshiriki mbio zozote hivi karibuni hadi watakapojiridhisha amepoma na hana tena maumivu ya misuli ya paja yaliyomkwamisha kwenye mbio za New York City Marathoni mwaka mwishoni mwa mwaka jana nchini Marekani ambako aliishia njiani.

“Hawezi kwenda Japan, atakapopona kabisa na kuwa fiti klwa ushindani tutamtafutia mbio atakazokwenda kushiriki na kufikia viwango vya dunia, lakini sio huko Japan,” alisema.

Kocha huyo alifafanua kwamba, kati ya Aprili na Mei, Simbu atakuwa yuko fiti kuchuana kusaka viwango vya kushiriki mbio za dunia.

“Tutamtafutia mbio za kufuzu kati ya miezi hiyo, huenda ikawa nchini Morocco au kwenye mbio zingine za Ulaya ambazo zinatambuliwa na Shirikisho la riadha la Kimataifa (IAAF).

Simbu bado hajafanya vyema tangu alipotoka kwenye kozi ya mwaka jana.