Kocha Simba awa gumzo

WAKATI wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Simba Mo  Arana , kocha mpya wa timu hiyo, Sven Vanderbroeck amekaa pembeni na daftari na kalamu akiandika kinachoendelea.
Msaidizi wake Seleman Matola ndiye anakiongoza kikosi hicho kwenye mazoezi hayo, huku bosi wake huyo akiwa anawafuatilia na kunoti kwenye daftari lake.
Pengine ni kwasababu ya ugeni kocha huyo anaonekana ni mpole tofauti na Patrick Aussems ambaye alikuwa akikinoa kikosi hicho, Sven aliwapungua mashabiki mkono ishara ya kuonyesha yupo pamoja nao.
Baada ya kocha huyo kushuka kwenye basi la timu alipita mbele ya mashabiki waliompokea kwa makofi na miruzi na kumwambia akaribie Tanzania, akawapungia mkono mara moja tu na kwenda kukaa sehemu aliyoandaliwa.

MASHABIKI WAMSHANGAA KOCHA
Nyomi ya mashabiki iliyofika kutazama mazoezi hayo, muda mwingi walikuwa wanamwangalia kocha huyo  kama watu wanaomtathimini halafu wanashindwa cha kufanya.
 Mjadala uliibuka kwa mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo walikuwa mchanganyiko wa Simba na Yanga na kuanza kuwazungumzia kocha mpya na wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera.
Wamesikika wakisema "Kocha mpole huyu sijui kachoka, yupo kimya kimya na daftari lake ngoja tuone," wamesikika wakisema.
Baadae akaanza kujadiliwa Zahera kwamba bora alivyotimuliwa wakiamini alikuwa ameishiwa mbinu
"Sisi mashabiki wa Yanga hatujaumia kuondoka kwa Zahera, kimbembe nyie msiyemwamini kocha wenu mpya," upinzani wa maneno ya mashabiki, wakibishana.