Kocha Simba alivyojilipua kwa AS Vita

Muktasari:

 

  • Niyonzima, Bocco wazungumzia mambo yalivyokuwa Simba kufuzu robo fainali

Dar es Salaam. Baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo kati ya Simba na AS Vita, mtu aliyekuwa na furaha zaidi kuliko mwingine ni Kocha wa Simba, Patrick Aussems ambaye unaweza kusema alijilipua na mambo yakajipa.

Mashabiki zaidi ya 50,000 waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa walikuwa wakimtazama atafanya nini kuivusha Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Simba iliyokuwa ikihitaji ushindi tu, ilipata bao dakika ya 87 lililofungwa na Clatous Chama na kuifanya Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 na kuipeleka timu hiyo robo fainali.

AS Vita ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 13 likifungwa na Francis Kazadi kabla ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kusawazisha dakika ya 35.

Miamba hiyo ya Tanzania imefikisha pointi tisa na sasa inaungana na Al Ahly yenye pointi 10 kusonga mbele na kuziacha JS Saoura iliyofikisha pointi nane wakati AS Vita iliyoingia fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, ikimaliza na pointi saba.

Simba na Al Ahly kutoka Kundi D zinaungana na miamba mingine kutoka Kundi A, Wydad Casablanca (Morocco) na Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini

Kundi B limetoa timu za Esperance ya Tunisia na Horoya ya Guinea wakati Kundi C ni TP Mazembe ya DR Congo na CS Costantine ya Algeria.

Aussems alivyojilipua

Wakati mchezo unaendelea, Aussems alikuwa amesimama akiwa haamini kinachoendelea, huku wachezaji wake wakijituma uwanjani.

Alichofanya ni kuwatoa Muzamiru Yassin, James Kotei na Emmanuel Okwi na kuwaingiza Hassan Dilunga, Rashid Juma na Haruna Niyonzima.

Uwanja uliguna na kukaa kimya kwa sekunde kadhaa wakati anatoka James Kotei ambaye alifanya kazi kubwa akisaidia ngome kuzuia mashambulizi ya akina Mundele Makusu, Fabrice Ngoma, Mukoko Batezadio, Emmanuel Ngudikama na wengine.

Alipojilipua sasa, kamtoa Kotei aliyesimama imara katika ngome akaingiza fowadi, Rashid Juma, kampunguza Okwi mbele akaingiza kiungo, Niyonzima ambaye hata hivyo aling’ara katikati na kufuta makosa ya Muzamiru ambaye awali alionekana kuzidiwa na kurudi nyuma.

Baada ya kutoka Okwi, hakukuwa na mguno mwingi, japokuwa ilionekana nguvu ya ushambuliaji ingepungua kwa kuwa Meddie Kagere na John Bocco sasa wanabaki wenyewe.

Niyonzima alitumia uzoefu, aliwapeleka puta AS Vita alianzisha mashambulizi katikati ya uwanja akipanda mbele na kurudi katikati kupokea mipira.

Alifanya hivyo kwa haraka na hata mpira uliozaa bao ulianzia kwake na kuutoa kwa Bocco ambaye alitaka kumrudishia naye akauacha na kumkuta Clatous Chama ambaye hakufanya ajizi.

Kimsingi, Aussems ni kama aliamua liwalo na liwe, alifahamu akifungwa au sare ametoka lakini akafanya uamuzi mgumu kwa wachezaji wake ambao wameleta matokeo chanya.

Akizungumzia mchezo huo, Aussems alisema ushindi wa vijana wake haukuja kama sapraizi ni mipango ya wachezaji na benchi la ufundi ambalo walitaka kushinda.

Alisema wamevuka na sasa wanaangalia mbele kwa kuwa hatua inayofuata ni ngumu zaidi, watajipanga kuhakikisha furaha ya ushindi inaendelea.

Niyonzima, Bocco wanena

Niyonzima aliwafunga midomo mashabiki waliokuwa wakiamini amepotea kisoka kwa kutokea benchi na kubadili upepo wa mchezo kiasi cha kuchangia ushindi wa Simba.

“Kocha aliponiambia nijiandae kuingia, alinituma nikafanye moja...mbili.. tatu.. siwezi kusema alichonituma sababu ni ‘technical issue’, nilimsikiliza huku nikimuomba Mungu anisaidie nikafanye kile alichonituma,” alisema Niyonzima jana alipozungumza na gazeti hili.

Kiungo huyo raia wa Rwanda ambaye amewafanyia sapraizi  mashabiki wa soka nchini kutokana na soka aliyoionyesha katika mchezo huo tangu alipojiunga na Simba ambako hakuwa na msimu mzuri baada ya kutoka Yanga.

“Unajua mpira una mambo mengi ila naweza kusema Mungu amenisaidia,” alisema Niyonzima.

Kiungo huyo ambaye mechi ya awali na AS Vita ya Congo aliingia kucheza dakika 20 za mwisho alisema, hakujali ambavyo alikuwa akiingia kucheza mwishoni.

“Sio na AS Vita pekee, mechi zote ambazo nilikuwa nikiingia mwishoni, wala sikujali, kwani siku zote niliamini mchezaji hata ukicheza dakika tano, kama una mchango katika timu utaonekana.

Mbali na Niyonzima, nahodha wa Simba, John  Bocco aliuzungumzia ushindi wa juzi akisisitiza ni hatua moja katika timu yao ambayo ina mikakati ya kufika fainali katika mashindano hayo kwa kuwa Simba ina kikosi imara cha ushindani.