Kocha Simba aibuka ataka pointi tatu za Ruvu Shooting

Muktasari:

Patrick Aussems hayupo nchini ikielezwa amerejea kwao kwa sababu binafsi huku presha ya klabu yake kumfuta kazi ikizidi kuongezeka.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ameibuka na kuelezea sababu za kuondoka kwake nchini na kwamba atarejea baada ya siku tatu.

Aussems aliondoka nchini jana ikielezwa amerudi kwao kwa siku mbili kwa sababu binafsi huku uongozi wa Simba ukisema kocha huyo aliwaaga akiwa Uwanja wa Ndege.

Leo Aussems akitumia ukurasa wake wa Mtandao wa kijamii wa Twitter na Instagram ameeleza kwamba ameondoka kwa sababu binafsi na atarejea nchini baada ya siku mbili.

Aidha Aussems ameeleza kwamba mara baada ya kurudi ataendelea na kazi yake akielekeza akili yake katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting katika kusaka pointi tatu.

Mapema mara baada ya Aussems kuondoka Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema wanatambua kuondoka kwa Aussems ingawa aliwaaga kwa barua pepe akiwa uwanja wa Ndege muda mfupi kabla ya kuondoka.

Inaelezwa kwamba Simba wanasubiri kurejea kwa kocha huyo ambapo huenda akakutana na kikao kizito cha kutakiwa kujieleza kufuatia hatua ya kuondoka kwake.

Hata hivyo kocha huyo atapishana na mchezo wa kirafiki utakaopigwa leo katika Uwanja wa Chamazi wakati Simba itakapokutana na JKT Tanzania ikiwa ni mechi ya pili tangu kupisha kalenda ya mechi za Kimataifa.

Mchezo wa kwanza wa kirafiki Simba ikicheza dhidi ya KMC ilipoteza kwa mabao 2-1 uliopigwa kwenye uwanja huo.

Simba hawaridhishwi na uwezo wa kikosi chao na inaelezwa ndani ya klabu yao huenda kuna mabadiliko yanaweza kufanyika katika benchi lao la ufundi ikiwamo kumuondoa kocha huyo Mbelgiji.