Kocha Simba agomea mastar wake kupanda lori

Muktasari:

Simba iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere saa 2:40 asubuhi kisha kuendelea kukaa ndani mpaka pale walipoanza kutoka saa 9:18 asubuhi.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck amegomea wachezaji wake kupanda gari la wazi lililoandaliwa maalum na uongozi wa klabu hiyo kwa lengo ka kutembeza kombe la ubingwa.

Simba iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere majira ya sa 2:40 asubuhi kisha kuendelea kukaa ndani mpaka pale walipoanza kutoka saa 9:18 asubuhi.

Kocha wa Simba ndiye aliyeanza kutoka nje ya vyumba vya uwanja huo na kuelekea upande yalipokuwa yamepaki magari ya mashabiki na gari maalum ambalo liliandaliwa kuwabeba wachezaji.

Kisha baada ya dakika moja akarudi tena ndani lakini wakati akiwa mlangoni akaonekana kuanza kuzozana na mwanadada Lispa Hatibu ambaye ni msaidizi wa ofisa Mtendaji mkuu wa Simba Senzo Mazingisa.

Mabishano hayo yalidumu kwa dakika moja kabla ya wahudumu wa uwanja na kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola kuwasihi waache ndipo Lispa alipoamua kuondoka kwa hasira huku akifoka.

Inadaiwa chanzo cha mzozo huo ni Sven kugoma wachezaji kupanda gari la wazi ambalo lilipangwa kupita katika barabara mbalimbali za Dar es Salaam mpaka makao makuu ya klabu hiyo Msimbazi huku yeye  akitaka timu kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Yanga itakayofanyika Jumapili.

Hata hivyo kocha Sven ni kama alishinda vita hiyo kwani alikomaa na msimamo wake wa kutoruhusu wachezaji kupanda gari la wazi hivyo wachezaji kupanda basi dogo la klabu hiyo aina ya Toyota Coaster.

Baada ya wachezaji kupanda basi, msafara umeanza kutoka uwanjani ukisindikizwa na mabasi yaliyobeba mashabiki na pikipiki