Kocha Namungo asimulia walivyoruhusiwa kutoka Rwanda na Kagere

Muktasari:

Janga la Corona limepelekea matukio mbalimbali ya kimichezo duniani kusimama ingawa Ujerumani tayari Ligi imerejea na nchini itaanza kati ya Juni 10 au 15 lakini kwa tahadhari.

Dar es Salaam.Baada ya kuwasili nchini jana usiku, kocha Thierry  Hitimana amesimulia namna walivyoruhusiwa kutoka nchini Rwanda akiwa na nyota wa Simba, Meddie Kagere.

Kocha huyo raia wa Rwanda alikwenda kwao baada ya Ligi kusimama nchini Tanzania Machi 17 ili kuchukua tahadhari ya janga la corona.

Amesema haikuwa kazi nyepesi kurejea Tanzania baada ya Rais Dk. John Magufuli kuruhusu michezo kuendelea Juni Mosi  kwani Rwanda imefunga mipaka kutokana na tahadhari ya janga la corona linalotikisa dunia.

"Hatukujua tutarudije, ila kuna mtu mmoja mkubwa tu kule Rwanda ndiye ametusaidia," amesema kocha Hitimana alipokuwa akizungumza na MCL Digital.

 

Amesema yeye na Kagere walimfuata wakamueleza namna wanavyopaswa kurejea kazini hivyo wakaruhusiwa kuvuka boda hadi kuingia Tanzania.

 

"Tumekuja na gari binafsi, ndege kule bado hazijaanza kuruhusiwa" amesema.