Kocha Mtunisia akabidhiwa Simba

Muktasari:

  • Kikosi cha Simba kimeanza mazoezi rasmi jana Jumatano huku kikiwakosa wachezaji wake watatu wa kigeni waliokuwa nje ya Tanzania, viungo Sharaf Eldin Shiboub aliyopo Sudan, Clatous Chama aliyepo Zambia na Francis Kahata ambaye yupo Kenya.

Benchi la ufundi la Simba limemuachia kibarua kizito kocha wa viungo, Adel Zrane kuendesha programu za timu hiyo katika maandalizi yao waliyoanza jana jijini katika Uwanja wa MO Simba Arena.

 Zrane amekabidhiwa kazi hiyo kwani ndiye husimamia mazoezi yote ya viungo na muda mwingi hufanya mazoezi ya nguvu na kufuatilia  kila mchezaji huko kocha mkuu, Sven Vandenbroeck akiwa pembeni anafuatilia.

Kwenye mazoezi hayo Simba, hutumia muda mwingi kufanya mazoezi ya nguvu kama kukimbia mbio ndefu na fupi, kutumia vifaa vya mazoezi kuruka na kulala, muda mwingine kubebana na mengineyo.

 Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamua alieleza kuwa hiyo ni ratiba ya timu ambayo wamejipangia ili kuhakikisha wanafanya mazoezi ya nguvu na kurudisha hali ya ufiti kwa wachezaji wao ambao muda mrefu walikuwa nyumbani.

"Kwa nini wanafanya mazoezi hayo ya nguvu kwa muda mrefu kuliko kuchezea mpira na Zrane ndio anasimamia hilo kocha mkuu ndio anaweza kueleza kwani ni masuala ya kiufundi zaidi hayo," anasema Rweyemamu.