Kocha Mtibwa hakuna kulala

BAADA ya juzi kuwachapa Azam FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, kikosi cha Mtibwa Sugar jana kilisafiri kwenda Bukoba kwa ajili ya mchezo wa raundi ya tisa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumza na Mwanaspoti, kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Vicent Barnabas alisema hawana muda wa kupoteza ndio maana wameamua kwenda Kagera mapema kutafuta pointi tatu muhimu.

“Mchezo unaofuata tunacheza na Kagera Sugar kule Bukoba moja ya timu bora kwenye ligi hii, kwa hiyo tumeamua kuwahi ili tupate muda wa timu kupumzika na kufanya mazoezi kwenye uwanja ambao tutachezea mechi,” alisema Vicent.

Pia, kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na klabu za Mtibwa, African Lyon na Yanga alieleza kuwa: “Wachezaji wanajitahidi kutekeleza mipango, mbinu na mikakati tofautitofauti tunayoielekeza mazoezini, hiyo ndio sababu kuu ya kupata pointi tatu, pia kujitoa kwao kuipambania timu ni jambo lingine linalotupa ushindi.”

Kabla ya kupewa timu ya Mtibwa Sugar, Barbanas alikuwa akikinoa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 cha timu hiyo na mpaka sasa ameshinda michezo yote miwili aliyokaa kwenye benchi kama kaimu kocha mkuu wa Mtibwa na kuifanya kufikisha pointi 11 ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, baada ya kucheza mechi nane kushinda tatu dhidi ya Ihefu 1-0, Namungo 1-0 na Azam 1-0, sare mbili na Ruvu Shooting 0-0, Simba 1-1 na imepoteza mechi tatu dhidi ya Yanga 1-0, Biashara 1-0 na Gwambina 2-0.