Kocha Mtibwa ajivua lawama kipigo cha Prisons

Wednesday January 9 2019

 

By Godfrey Kahango

Mbeya. Kocha wa Mtibwa,  Zubeiry Katwila amesema ushindi wa Prisons dhidi  ya timu yake ya Mtibwa wa mabao 2-0 jana Jumanne ulitokana na umakini wa wachezaji wao, lakini wachezaji upande wao walikosa umakini hususani kwenye umaliziaji mipira ya mwisho.

Alisema hawakuwadharau Prisons kutokana na mwenendo wake wa sasa katika ligi, bali ushindi walioupata ni wa halali.

Alisema, “Bado wapo vizuri lakini wachezaji wangu walikosa umakini, ila wenzetu wamepata nafasi na wamezitumia vyema kabisa,” amesema Katwila.

Tanzania Prisons wameanza kuonesha matumaini ndani ya klabu hiyo baada ya kuitandika Mtibwa Sugar mabao 2-0 kwenye ya Ligi Kuu Bara iliyochezewa jana Jumanne Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Prisons imepata ushindi huo ikiwa ni wa pili kati mechi zote 21 ilizocheza tangu kuanza kwa ligi hiyo huku mechi nyingine ilikuwa ikipoteza au kutoa sare.

Mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Salumu Kimenya dakika ya 71 akipokea pasi kutoka kwa Jumanne Elfadhili baada ya mpira uliokuwa umepigwa na Jeremiah Juma kupanguliwa na kipa wa Mtibwa Shaban Kado.

Bao la pili lilipatikana kiwa njia ya mkwaju wa penati iliyopigwa na Jumanne Elfadhili dakika ya 90. Penati hiyo ilitokana na mlinzi wa Mtibwa Sugar Dickson Job kumchezea rafu mshambuliaji wa Prisons Adam Adam eneo la hatari wakati akiwa kwenye harakati za kuelekea kwenye lango la Mtibwa.

Hata hivyo, mwamuzi wa kati Mbaraka Rashid kutoka Dar es Salaam alilazimika kumpatia kadi nyekundu mchezi wa Mtibwa Japhary Kibaya dakika za mwisho baada ya kumchezea  rafu mchezaji wa Prisos, Jumanne Elfadhil.

 

Advertisement