Kocha Mbao aivutia kasi Everton

Muktasari:

Beki huyo wa zamani wa Simba, alisema mashindano hayo hayawezi kuharibu programu yake ya mafunzo kwa kuwa ana kikosi kipana kinachoundwa na wachezaji wenye viwango bora

Mwanza. Kocha wa Mbao Amri Said, amesema ana ndoto ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya SportsPesa msimu huu.

Said alisema anatarajia kutumia kikosi cha kwanza katika mashindano hayo ili kupata uzoefu ambao utatumika kushindana katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Pia alisema mkakati wake ni kutwaa ubingwa wa SportsPesa ili kupata nafasi ya kucheza mechi ya kimataifa na Everton ya England.

Kocha huyo alisema kushiriki mashindano hayo ni fursa na wataitumia vyema kucheza kwa umakini.

Beki huyo wa zamani wa Simba, alisema mashindano hayo hayawezi kuharibu programu yake ya mafunzo kwa kuwa ana kikosi kipana kinachoundwa na wachezaji wenye viwango bora.

“Tutaonyesha ubora wetu nina kikosi kipana na vijana wana uwezo, lazima tutwae ubingwa na kujitangaza kimataifa,”alisema Said.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli alisema Mbao inawakilisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa katika mashindano, hivyo itacheza kwa kiwango bora ili kuweka rekodi mpya.