Kocha Kurasini Heat atoa siri ya ubingwa

Dar es Salaam. Ushindi wa tofauti ya pointi tatu kwenye mchezo wa nne wa fainali umeipa Kurasini Heat ubingwa wa ligi ya mpira wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), huku kocha, Shendu Mwagalla akianika kilichowabeba.

Kurasini imetawazwa kuwa bingwa mpya wa RBA juzi usiku baada ya kuichapa JKT kwa pointi 64-61 katika mechi ya nne (game four) ya fainali kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini.

Kwa matokeo hayo, Kurasini Heat imeibuka bingwa kwa ushindi wa mechi 3-1, katika mechi zote zilizokuwa na ushindani kwa timu zote.

Kurasini ilipata tabu katika hatua ya nusu fainali, ilipolazimika kucheza mechi tano (game five) na ABC, ambayo ilitoa upinzani mkubwa kwa mabingwa hao wapya wa Dar es Salaam katika kikapu.

Timu hiyo ambayo ilianza kwa kufungwa pointi 64-57, ilipindua meza kwenye mechi ya pili (game two) na kushinda... ikivunja rekodi ya JKT ya kutofungwa msimu huu katika mechi 21 ilizocheza ikiwamo 15 za ligi, mbili za robo fainali na tatu za nusu fainali.

Kurasini Heat ilishinda mechi ya pili mfululizo kwa pointi 78-77 kabla ya juzi usiku kushinda pointi 64-61 na kutawazwa kuwa bingwa mpya wa RBA mwaka huu.

“Tuliwasoma JKT, tukabaini ina wachezaji wake tegemeo,tuliweka nguvu kubwa kuwadhibiti wachezaji hao, tulikubaliana hata kama watafunga, basi wasifunge kwa uhuru, hivyo safu yetu ya ulinzi ilicheza ‘man to man’,” alisema kocha huyo.

Mwagalla alisema kingine kilichowabeba ni kocha wa JKT katika mechi hiyo muda mwingi akuutumia kulalamikia waamuzi wa mchezo huo, jambo ambalo kitaalamu lilimtoa kwenye mchezo huo mgumu.

“Pia mchezaji wao, Mussa Chacha (ni nahodha), alifanya faulo na kupewa kadi nyekundu kwenye ‘game one’, aliigharimu timu, kwani ni mmoja wa nyota tegemeo wa JKT,” alisema.

Katika mechi hiyo, JKT iliongoza robo ya kwanza, kabla ya

Kurasini Heat kurudisha robo ya pili na robo ya tatu timu hizo zilikuwa na pointi 51-51.

Robo ya nne sekunde chache kabla ya mechi kumalizika timu hizo zilikuwa na pointi 61-61 kabla ya Kurasini Heat kupata faulo na kufunga pointi moja, na sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho ikaongeza pointi nyingine mbili.

Kurasini Heat imetwaa ubingwa huo baada ya kuusote kwa miaka 11 bila kutinga fainali, msimu huu imekuwa fainali yao ya kwanza kucheza na kutwaa ubingwa.

Hayo ni mafanikio makubwa kwa Mwagalla, ambaye amekuwa na msimu nzuri katika kuimarisha kikosi kuanzia mwanzo wa mashindano hadi mwisho.

Anaingia katika rekodi baada ya kuifunga JKT, ambayo ilikuwa na msimu mzuri kwa kucheza mechi 15 bila kupoteza wowote kwenye mashindano ya msimu huu hatua ya awali.