Kocha Kikapu apewa kibano

Muktasari:

  • Alisema kutokana na changamoto hizo, kikao cha kamati ya utendaji ya TBF kimeamua kocha huyo asimamishwe kuratibu masuala ya 3x3 nchini hadi itakapoamuliwa vinginevyo.

Dar es Salaam. Kocha wa mpira wa kikapu nchini, Karabani Karabani amesimamishwa kujihusisha kuratibu masuala ya mchezo huo kwa timu ya Taifa ya 3x3.

Kocha Karabani alikuwa mratibu wa mchezo huo mpya wa mpira wa kikapu nchini ambao unashirikisha wachezaji wanne ambao watatu ndiyo wanacheza na mmoja anakuwa mchezaji wa akiba.

Rais wa Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa amesema uratibu wa Kitaifa wa mchezo huo utasimamiwa na kocha, Robert Manyerere na Mohamed Tasso.

"Makocha hawa wanatakiwa kuhakikisha mikoa yote inajua kanuni, taratibu na sheria za 3x3 na  mashindano yetu yote ya Kitaifa yanashirikisha pia mchezo wa 3x3 na timu zetu zote za Taifa zinaa andaliwa vizuri kwa ajili ya mashindano ya Kimataifa," alisema.

Akizungumzia kufungiwa kwa kocha Karabani, Magesa alisema alishindwa kutimiza wajibu wake katika maandalizi ya timu ya Taifa ya Kikapu ya U18 ya 3x3 iliyoshiriki mashindano ya Kimbari nchini Rwanda, kulingana na maelekezo ya Serikali, TOC na TBF.

Alisema kocha huyo aliwapigia simu wachezaji wa timu hiyo ya Taifa na kuwashawishi wasiende kambini Kibaha, suala hili lilisababisha timu kuchelewa kufika kambini na kusababisha kuchelewa kupata vifaa vya michezo.

"Hiyo haikuwa mara ya kwanza, kwani mwaka jana pia kocha Karabani alishindwa kutimiza wajibu wake katika maandalizi ya timu ya Taifa ya Kikapu ya U18 ya 3x3 na kusababisha timu hiyo kutoshiriki mashindano ya Afrika ya 3x3 wakati tukiwa tumefuzu," alisema Magesa.

Alisema kutokana na changamoto hizo, kikao cha kamati ya utendaji ya TBF kimeamua kocha huyo asimamishwe kuratibu masuala ya 3x3 nchini hadi itakapoamuliwa vinginevyo.