Kocha Katwila atua Mwanza aipigia hesabu kali Mbao

Muktasari:

  • Mchezo huo ni wa raundi ya 10 kwa timu hizo, Mtibwa Sugar wapo nafasi ya pili kwa pointi 17, huku Mbao FC wakiwa wamevuna alama 14 na kukaa nafasi ya 17. Pia Mbao kati ya mechi tatu ilizocheza uwanja wake wa nyumbani imeshinda mbili na kupoteza moja.

MWANZA. Mtibwa Sugar wajanja wamekaa na kusikiliza tambo za Mbao FC kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu utakaopigwa keshokutwa Jumapili jijini Mwanza na kutamka kuwa wapinzani hao wajiandae kwa kichapo.
Timu hizo zitarajia kujitupa kwenye Uwanja CCM Kirumba jijini hapa, huku rekodi ikionyesha mechi ya mwisho msimu uliopita hazikufungana, lakini Mtibwa waliwahi kulazwa mabao 5-0 msimu wa 2016/17.
Kocha Mkuu wa Mtibwa, Zubery Katwila alisema hana wasiwasi na kikosi chake kutokana na morali waliyonayo na kwamba wanakuja kwa lengo la kuchukua pointi tatu na kusepa.
Alisema kuwa licha ya kwamba anaamini mchezo utakuwa na ushindani kwani Mbao iliwahi kuichapa Mtibwa mabao 5-0 wakiwa katika uwanja huo, lakini mbinu atakazotumia lazima wapinzani waumie.
“Tupo vizuri na tumejipanga kushinda mchezo huo vijana wote wana ari na hakuna atakayekosa mechi hiyo,japo mchezo utakuwa na ushindani kwa sababu Mbao wapo nyumbani ila lazima tushinde,” alisema Katwila.
Mshambuliaji Juma Liuzio alisema mkakati wao ni kushinda mpambano huo ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu.
Alisema kuwa Mbao wanawaheshimu, lakini hawawapi presha na kwamba kikubwa ni kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi ili kuhakikisha wanapata walichokilenga.
“Ni mchezo mzuri na wenye ushindani kwa sababu Mbao ni wazuri lakini sisi ni zaidi,tunataka ushindi ili kuendelea kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema nyota huyo wa zamani wa Simba.