Kocha Kagera Sugar afichua nyota wake wanamwangusha

Muktasari:

  • Jangalu alisema umakini mdogo kwa wachezaji na kujichanganya kwa mabeki wao ndio sababu za kupoteza mchezo huo muhimu ambao ungewapa pointi tatu na kujiweka nafasi nzuri.

MWANZA.KOCHA Msaidizi wa Kagera Sugar, Ally Jangalu ameeleza sababu za kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa nyumbani wa Kaitaba wachezaji wao kupoteza umakini uwanjani.

Timu hiyo ya mjini Bukoba kwa sasa hali yake si shwari kwani inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 na miongoni mwa timu zinazochuana vikali kukwepa kushuka daraja.

Jangalu alisema umakini mdogo kwa wachezaji na kujichanganya kwa mabeki wao ndio sababu za kupoteza mchezo huo muhimu ambao ungewapa pointi tatu na kujiweka nafasi nzuri.

Alisema benchi la ufundi linajipanga upya kuhakikisha mapungufu hayo wanayafanyia kazi ili mechi zinazofuata wapate ushindi na kujiimarisha kwenye msimamo. Straika wa timu hiyo, Christopher Edward ‘Edo’ alikiri ugumu wa ligi na timu inayofanya makosa kidogo wapinzani wao wanaitumia kama fursa kushinda.

Alisema hakuna namna nyingine zaidi ya kila mmoja kwa nafasi yake kuonyesha uwezo na umakini katika michezo iliyobaki ili kuhakikisha wanashinda na kubakia nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.