Kocha Ihefu aibukia Ligi Daraja la Kwanza

Muktasari:

Gipco inashika nafasi ya nne katika msimamo wa kundi A la Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na pointi nne

Kocha aliyeachana na Ihefu ya Mbeya hivi karibuni, Maka Malwisi amejiunga rasmi na klabu ya Gipco ya Ligi Daraja la Kwanza kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Timu hiyo ya Gipco ipo katika mchakato wa kubadili jina na kuanza kuitwa Ken Gold baada ya kuuzwa kutoka mkoani Geita na kuhamia huko Chunya, Mbeya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malwisi ambaye msimu uliopita aliiongoza Ihefu kupanda daraja, alisema kuwa leo amejiunga rasmi na Gipco na lengo lake kuu ni kuhakikisha inapanda Ligi Kuu.

"Ni kweli nimesaini mkataba wa kuitumikia timu hii kwa mkataba wa mwaka mmoja na baada ya hapo tunaweza kukaa mezani tena na kuongeza ikiwa malengo tuliyoweka yatatimia.

Kikubwa timu nimeona imefanya vizuri na imejitahidi kweli katika michezo yake iliyopita na ni nzuri hivyo nina imani kubwa tutafanya vyema," alisema Malwisi.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Ihefu iliamua kuachana na Malwisi kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu na nafasi yake kuchukuliwa na Zubery Katwila aliyekuwa Mtibwa Sugar.

Hadi anaondoka Ihefu, Malwisi alikuwa ameiongoza timu hiyo kukusanya jumla ya pointi tatu katika mechi tano ilizokuwa imecheza

Gipco inashika nafasi ya nne katika msimamo wa kundi A la Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na pointi nne ambazo imekusanya baada ya kushinda mechi moja, kutoka sare moja na kupoteza moja