Kocha Hodgson anogewa Crystal Palace

Friday August 10 2018

 

London, England. Kocha wa zamani wa England, Roy Hodgson, amesaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi kuinoa Crystal Palace.

Kocha huyo mwenye miaka 71, alianza kuinoa Crystal Palace, Septemba 2017 ikiwa katika janga la kushuka daraja ikiwa imecheza mechi saba bila kushinda lakini akaiwezesha kumaliza Ligi katika nafasi ya 11.

Kocha huyo aliyeshindwa kupata mafanikio akiwa na Liverpool sasa atakaa Selhurst Park hadi mwisho wa msimu wa mwaka 2019-20.

"Ninayo furaha kuongeza mkataba wa kuendelea kuwa hapa Crystal Palace, tangu nimeanza kazi hapa nimekuwa na mafanikio na uungwaji mkono wa kutosha,” alisema Hodgson.

Alisema anawashukuru viongozi na mashabiki wa klabu hiyo kwa kumuunga mkono jambo lililochangia kupatikana mafanikio hayo.

Naye mwenyekiti wa klabu hiyo, Steve Parish alisema wanajivunia kufikia makubaliano na kocha huyo ambaye ameifanya klabu yao kupiga hatua kisoka na wana matarajio ya kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Timu hiyo leo itaanza kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kucheza na timu iliyorejea Ligi Kuu England ya Fulham.

 

Advertisement