Kocha Hitimana apumua Namungo

Dar es Salaam. Kuimarika kwa wachezaji nyota watatu wa Namungo FC kumeonekana kumshusha presha kocha Thiery Hitimana wa timu hiyo.

Kocha huyo, ambaye msimu ujao atakiongoza kikosi hicho kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, alisema wingi wa majeruhi kwenye kikosi chake ulikuwa ukimtesa katika kuboresha kikosi.

“Hivi sasa naona mwanga, kwani majeruhi wengi wameanza kuimarika, na kurudi mazoezini kuungana na wenzao,” alisema Hitimana.

Aliwataja wachezaji waliopona kuwa ni mabeki, Carlos Protas na Edward Manyama sanjari na mshambuliaji wa kati raia wa Ghana, Stephen Sey.

Kocha huyo raia wa Burundi alisema kuimarika kwa wachezaji hao kumepanua wigo zaidi kwenye mazoezi, ingawa bado beki Abeid Athuman na Adam Salamba hawako fiti.

“Nimebaki na majeruhi wawili pekee, japo wakati ligi inaanza tulitengeneza majeruhi wengi, hatukuwa na muda wa maandalizi.

“Hii ilinipa shida kidogo ligi ilipoanza, wingi wa majeruhi ulitusumbua, wachezaji zaidi ya saba walikuwa majeruhi, ingawa sasa wote wameimarika isipokuwa Salamba na Abeid pekee,” alisema kocha huyo.