Kocha Foutain Gate kaanza tambo

TAYARI Fountain Gate imenza jeuri huko Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ikiwa ni baada ya kuiangushia kichapo cha maana Alliance FC kwenye mchezo wa kwanza cha mabao 3-0.

Fountain Gate ni kinara wa kundi B ikiwa na alama tatu na mabao matatu japo inategemea na matokeo ya mchezo wa jana kati ya Rhino Rangers na Mbao FC

Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema kila kitu kinategemeana na mipango ambayo wamejiwekea kuhakikisha wanfanya vizuri kwenye ligi. “Sina kitu cha zaidi ya kuwapongeza vijana wangu kwa namna ambavyo wanajituma na kufuata yale ninayowaelekeza kuyafanya uwanjani,” alisema Muya.

“Safari bado ndefu ya kuhakikisha tunaendelea kubaki nafasi tuliyokuwa nayo, japo najua haitakuwa kazi ndogo, lakini kikubwa ni kuendelea kupambana na wapenzi wetu wazidi kutupatia sapoti.”

Aliongeza kuwa kila mchezo kwao wanakuwa na mbinu tofauti kutokana na wapinzani wanaowakabili, ndio maana huwasisitiza vijana wake kuwaheshimu.

Fountain Gate ilipanda daraja na kufanikiwa kuwa bingwa wa Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya kuichapa 2-1 Kitayosce msimu uliopita kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa.