Kocha Emery amtuma mabao Aubameyang

Thursday December 6 2018

 

LONDON, ENGLAND . KOCHA Unai Emery amempa kazi ngumu fowadi wake, Pierre-Emerick Aubameyang kuwa anamtaka ashinde Tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England kwa msimu huu.

Aubameyang ameonekana kuwa moto kwenye ligi hiyo akitikisa nyavu kama anavyotaka tangu alitua Emirates Januari mwaka huu na msimu huu yeye ndiye kinara wa kufunga akiwa ameweka kambani mabao 10.

Jumapili iliyopita, staa huyo wa Gabon alifunga mara mbili dhidi ya Tottenham na usiku wa jana Jumatano alitazamiwa kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England huko uwanjani Old Trafford. Kuhusu Auba tangu alipotua Arsenal akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya Pauni 56 milioni, amefunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu England.

Msimu uliopita, staa wa Liverpool, Mohamed Salah, ndiye aliyenyakua Kiatu cha Dhahabu na mabao yake 32, lakini msimu huu mambo yanaonekana kugeuka na Aubameyang anapewa nafasi kubwa ya kuibeba tuzo hiyo.

Emery alisemas: “Namtaka aendelee kuboresha kiwango chake na kushinda tuzo binafsi. Nimempa mtihani wa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England msimu huu. Tutakachofanya ni kumsaidia kulifanikisha hilo kwa sababu tunafahamu kama akiwa anafunga mabao yatatusaidia sisi.”

Advertisement