Kocha Chelsea anakomaa usajili

Wednesday September 16 2020

 

London, England. Chelsea imeripotiwa kuwa na mpango wa kupiga bei mastaa wanne ili kupata pesa itakayotosha kunasa saini ya kiungo Declan Rice kutoka West Ham United.

The Blues chini ya kocha Frank Lampard kwa sasa imehamishia nguvu kwenye usajili wa Rice baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili kipa Edouard Mendy, ambaye anaweza kutambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Chelsea muda wowote kutoka sasa.

Hata hivyo, kuhusu Rice, West Ham United inaripotiwa kwamba inahitaji mkwanja usiopungua Pauni 70 milioni ili kumruhusu mchezaji huyo aondoke, kiwango ambacho The Blues hawapo tayari kulipa kwa sasa.

Taarifa nyingine imedai kwamba kutokana na kocha kocha Lampard ameamua kuweka sokoni baadhi ya wachezaji wake ili kupata pesa ya kusajili baada ya sasa kuwa ametumia zaidi ya Pauni 200 milioni kwenye usajili wa mastaa wapya katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye orodha hiyo ya wachezaji wanne, yupo Jorginho, Tiemoue Bakayoko, Danny Drinkwater na Andreas Christensen. Ujio wa wachezaji Kai Havertz na Thiago Silva unamfanya Lampard aamini kwamba wachezaji hao wanne hawatakuwa na umuhimu tena wa kuwapo kwenye kikosi chake, hivyo ni sawa tu wakiondoka.

Chelsea ndiyo timu iliyofanya usajili wa pesa nyingi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuwanasa Hakim Ziyech, Timo Werner, Ben Chilwell, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Havertz na beki wa kati mkongwe, Silva.

Advertisement

 

 

Advertisement