Mastraika Stars wamkera Bilal

Wednesday December 6 2017

 

By MASOUD MASASI

Mwanza. Kili Stars ilianza michuano ya Kombe la Chalenji vibaya baada ya kupata suluhu na Libya huku mastraika wake, Elius Maguli, Mbaraka Yusuf na Danny Lyanga wakikosa mabao ya wazi jambo ambalo limemkera kocha wa zamani wa  Stand United, Athuman Bilal 'Bilo'.
Bilo ambaye sasa yuko mapumzikoni baada ya kusimamishwa na Stand United alisema washambuliaji wa Kilimanjaro wasipombana basi timu hiyo itaishia katika hatua ya makundi jambo ambalo ni aibu kubwa kwa nchi yetu.
“Nimeangalia mchezo wao na Libya, kocha anatakiwa arekebishe safu ya ushambuliaji bado kuna tatizo kubwa la umaliziaji  na hili ni jambo baya kwani hatutoweza kufika mbali hali hii ikiendelea,” alisema Bilo.
Akizungumzia hatima yake ndani ya Stand United, alisema anachotambua ni kwamba bado yeye ni mwajiriwa wa klabu hiyo na anachotumikia kwa sasa ni adhabu ya kusimamishwa tu.