Kocha Biashara aitisha Yanga

BIASHARA United haijawahi kufungwa na Yanga nyumbani tangu ipande Ligi Kuu 2018, lakini kocha wa kikosi hicho, Francis Baraza amesisitiza kwamba Jumamosi kitanuka kwani hawatakubali.

Baraza amekiri kuwa baada ya kumaliza mechi na Polisi Tanzania waliyoshinda kwa bao 1-0, jioni alivuta kiti na kutulia kwenye tivii na kuisoma Yanga ilipokuwa ikicheza na KMC.

Timu hiyo tangu ipande daraja imekutana na Yanga mara mbili kwenye Uwanja wao wa Karume uliopo Musoma mkoani Mara, huku ikishinda mara moja kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Mei 10, mwaka jana na mchezo mwingine kutoka suluhu msimu uliopita.

“Itakuwa moja ya mechi ngumu kwani Yanga hivi sasa wako vizuri na ujio wa kocha mpya (Cedrick Kaze) umeongeza kitu katika kikosi hicho, kwani hata ukiwaona kuna mabadiliko ya kiuchezaji sio kama mwanzo. Hivyo itakuwa vita kubwa ndani ya dakika 90 kwani hata sisi hatutakubali kupoteza dhidi yao tena kwenye uwanja wetu wa wa nyumbani,” alisema.

“Nimeshawasoma vizuri na kubaini ubora na udhaifu wao, hivyo tutaanza kuipangia mikakati ya pointi tatu Jumanne hii (leo) tutakaporejea mazoezini Uwanja wa Karume. “Ushindi dhidi ya Polisi Tanzania umerudisha morali katika kikosi changu kwani kabla ya hiyo mechi tulipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Coastal. Kilikuwa kipigo kikubwa sana ambacho hatukitarajia na kilituvuruga.”