Kocha Biashara United asaka mshambuliaji wa mkopo

Muktasari:

Biashara United ilipanda daraja msimu huu, ina pointi 10 katika msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo 13, imeshinda mmoja, imetoa sare michezo saba na imepoteza mitano huku ikishika mkia kwenye msimamo wa ligi.

Dar es Salaam. Kocha wa Biashara United, Hitimana Thiery amesema anataka kusajili wachezaji watatu akiwemo mshambuliaji mmoja, kiungo mshambuliaji na beki katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Novemba 15 na litafungwa Desemba 15.

Biashara United imeanza Ligi Kuu kwa kusuasua ikiburuza mkia baada ya kucheza michezo 13, ikitoka sare saba, kufungwa mitano na kushinda mechi mmoja.

Akizungumzia kikosi chake Hitimana alisema ukiangalia sababu kubwa ambayo imesababisha kufanya vibaya katika michezo yetu 13 tuliyocheza mpaka sasa ni kukosa mshambuliaji na kiungo mshambuliaji walio sawasawa.

"Nina mawinga wazuri katika timu yangu pia hata viungo ninao wazuri kiasi lakini nakosa watu wa mwisho wanaoweza kutumbukiza mpira wavuni na timu ikapata ushindi," alisema Mrundi Hitimana.

Hitimana alisema anasaka wachezaji hao katika timu yoyote inayoshiriki ligi za madaraja mbalimbali ingawa itapendeza zaidi akiwapata kwa mkopo kutoka timu za Ligi Kuu.

"Hivi sasa ni kipindi cha usajili, nimeshaongea na viongozi wangu kuona tunawapataje wachezaji hao ninaowataka.

"Najua kuna timu hasa kubwa kuna wachezaji haziwatumii na zinaweza kuwatoa kwa mkopo hivyo kama tutafanikiwa kuwapata baadhi yao itakuwa vizuri kwa sababu tayari watakuwa wana uzoefu wa ligi na watatusaidia,"alisema Hitimana.