Kocha Azam agawa programu ya mazoezi

Muktasari:

Cioaba alisema programu hiyo inamuelekeza kila mmoja kwa namna yake kufanya mazoezi hayo ili awe fiti mpaka hapo watakaporejea.

Dar es Salaam.Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba amesema kipindi hiki ligi imesimama hawajawaacha wachezaji wake hivi hivi badala yake amewapa programu maalumu ya kufanya kila mmoja anapokuwa yupo nyumbani kwake.

Cioaba alisema programu hiyo inamuelekeza kila mmoja kwa namna yake kufanya mazoezi hayo ili awe fiti mpaka hapo watakaporejea.

"Nimewapa wachezaji wangu programu hizo muhimu ili wawe fiti muda wote, ligi imesimama na hakuna aliyependa lakini ni tatizo limetokea Duniani hivyo hakuna jinsi zaidi ya kulikabili," alisema.

Mromania huyo alisema sehemu mojawapo ya programu hiyo ni kuhakikisha unakimbia unapokuwa nyumbani au kufanya mazoezi ya Gym.

"Unatakiwa ukimbia na kuna namna ya maelekezo ambayo yapo katika kila programu, hukimbii tu kwamba unakimbia kuna namna ya kukimbia, dakika 10 halafu unayoosha na mazoezi madogo madogo," alisema.

"Kama hauwezi kupata Gym sehemu uliyopo basi unaweza ukafanya skwashi kulingana na dakika zilizopo," alisema.

Aliongeza kwa kusema amekuwa na ukaribu wa hali ya juu na meneja wa timu hiyo kuona mrejesho wa kila mchezaji.

"Meneja amekuwa akiwasiliana na wachezaji kila siku kujua hali zao kisha kunipa mrejesho, nafurahi kuona wanaendelea salama," alisema.

Naye kiungo wa timu hiyo, Never Tigere ambaye yupo nchini Zimbabwe, alikiri kupokea programu maalum na ndiyo anaifanyia kazi.

"Tuna programu zetu za kufanya mazoezi ndio huwa yunajifua nazo, ni nzuri inatuweka fiti hata tukiwa nyumbani," alisema.

Ligi nyingi zimesimama baada ya virusi vya corona kusambaa na kuua maelfu ya watu duniani.