Kocha Aussems aingia mitini, Al Ahly yatamba

Muktasari:

  • Kesho Jumanne Simba watakuwa nyumbani kuwakaribisha Al Ahly katika mechi ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameingia mitini katika mkutano na vyombo vya habari huku mwenzake wa Al Ahly, Martin Lasarte akitamba kuondoka na ushindi katika mechi ya kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mkutano huo ni kawaida kwa kila timu kuwakilishwa na kocha mkuu pamoja na nahodha au mchezaji yeyote.

Katika jambo la kushangaza kocha Aussems hakutokea na badala yake alikuja kocha wa makipa Mwarami Mohammed 'Shilton' ambaye alikataliwa kuzungumza na kiongozi wa CAF aliyekuwa hapo kwa kumueleza anayeruhusiwa ni kocha mkuu.

Baada ya kuzuiliwa Mwarami kuzungumza jukumu la kuizungumzia mechi hiyo lilibebwa na nahodha msaidizi Mohamed Hussen ‘Zimbwe Jr’.

Nahodha Zimbwe alisema mechi itakuwa ngumu na wanatambua umuhimu wa mchezo huo kwao wachezaji.

Alisema mashindano haya kila timu inatumia uwanja wake wa nyumbani basi hata kwetu tumejipanga kufanya hivyo.

"Siwezi kusema kocha ametupa mbinu zipi, lakini kama wachezaji kwetu tumejipanga kupata pointi tatu," alisema Zimbwe.

Naye kocha wa Al Ahly, Lasarte alisema mechi ya kwanza ambayo walishinda 5-0, imebaki historia na wanachoangalia ni mechi hii ambayo kama watashinda watafuzu hatua ya robo fainali.

Anasema tunafahamu tunacheza mechi ugenini, lakini yaliyotokea katika mechi iliyopita imebaki historia na tunachoangalia ni kupata matokeo ya ushindi ugenini.

"Hali ya hewa ni tofauti na ya kwetu, lakini muda tuliofika tunajitahidi kuzoea na kufanya mazoezi katika hali hii ili kutumiza malengo," alisema.

"Nimepata muda wa kuwafuatilia Simba kwa kuangakia video," alisema.

Al Ahly iwapo itashinda mchezo huo itakuwa imejihakikishia kufuzu kwa hatua ya robo fainali.