Kocha Arsene Wenger aisubiri Bayern na PSG

Muktasari:

Kocha wa zamani wa Arsenal Wenger hana kibarua tangu atimuliwe kijanja na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita baada ya miaka 22 ya kufanya kazi Highbury kisha Emirates akiwa na wababe hao wa London baada ya kuondoka Arsenal na aliikataa Fulham ambayo ingemfanya aendelee kuishi tena London kwa mara nyingine.

LONDON, ENGLAND. CLAUDIO Ranieri amechaguliwa kuwa kocha mpya wa Fulham baada ya klabu hiyo ya London kufukuza kocha wake Slavisa Jokanovic, lakini kabla Ranier hajapewa kazi hiyo kumbe kibarua kilikwenda kwa Mzee Arsene Wenger akawapa jibu moja tu. Hapana.

Fulham imemfukuza Jokanovic baada ya kufanya vibaya licha ya kuchukua wachezaji 12 wapya ilipopakupanda Ligi Kuu msimu huu na kutumia takribani Pauni 100 katika dirisha la usajili.

Na akili ya kwanza ya tajiri wa timu hiyo, Shahid Khan ilikuwa ni kumchukua Wenger.

Wenger hana kibarua tangu atimuliwe kijanja na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita baada ya miaka 22 ya kufanya kazi Highbury kisha Emirates akiwa na wababe hao wa London na nafasi yake imekwenda kwa Kocha Mhispaniola, Unai Emery Inadaiwa kocha huyo Mfaransa anashikilia msimamo wake wa kutofundisha timu nyingine yoyote ya England baada ya kuondoka Arsenal na aliikataa Fulham ambayo ingemfanya aendelee kuishi tena London kwa mara nyingine.

Tajiri wa Fulham, Khan anaelewana sana na mmliki wa Arsenal, Stan Kroenke, ambaye ndiye aliyempa sifa za Wenger. Siku zote Kroenke amekuwa shabiki mkubwa wa Wenger ingawa hatimaye kwa shinikizo la watu wake wa karibu aliamua kuachana na kocha huyo Mei, mwaka huu.

Achilia mbali Wenger, makocha wengine ambao walikataa kazi ya Fulham ni pamoja na kocha wa zamani wa Monaco, Leonardo Jardim, ambaye aliondoka Monaco hivi karibuni baada ya kuiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ufaransa miaka miwili iliyopita huku pia akiipeleka katika hatua nusu fainali michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha mwingine ambaye alikataa fursa ya kuiokoa Fulham isishuke daraja ni kocha wa zamani wa Chelsea na Tottenham, Andre Villas-Boas.

Kocha huyo Mreno ambaye hakuacha jina kubwa England kwa sasa yupo katika Klabu ya Shanghai SIPG ya Ligi Kuu China na mkataba wake unatarajiwa kumalizika Novemba mwaka huu.

Inaeleweka Wenger anasubiri kazi nyingine nje ya England ambapo inasemekana anainyatia kwa kasi kazi ya Bayern Munich inayoweza kumfukuza kocha wao, Niko Kovac kufuatia mwanzo mbovu wa klabu hiyo kwenye Bundesliga.

Mpaka sasa Bayern Munich inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya Ujerumani huku wakiwa nyuma kwa pointi saba mbele ya Borussia Dortmund na kuna wasiwasi ndani ya mechi tatu kama, Kovac hatarekebisha mambo basi huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Mapema mwezi uliopita, Wenger alithibitisha anajiandaa kurudi tena katika kiti cha ukocha ingawa hakuweka wazi ni katika klabu gani au katika ngazi gani ya ukocha.

“Naamini nitaanza tena Januari Mosi. Kwa miaka yangu 22 nina uzoefu mkubwa katika ngazi tofauti. Kuna watu wananihitaji. Kuna vyama vya soka, timu za taifa, inaweza kuwa hata Japan,” alisema kocha huyo Mfaransa.

PSG inadaiwa inamtaka, Wenger awe mkurugenzi wa ufundi juu ya kocha wake wa sasa, Thomas Tuchel na haijulikani kama, Wenger anatamani kazi hiyo au anataka kurudi tena katika benchi la ufundi moja kwa moja kama zamani.