Kocha Alliance awaibukia mazoezini wachezaji wake

Kocha Habibu Kondo mwenye tisheti nyekundu akiwa mazoezini na timu ya Alliance FC

Muktasari:

Kocha huyo alikosekana katika mchezo wao uliopita dhidi ya  Yanga,ikiwa ni siku chache baada ya Alliance kupokea kipigo cha mabao 5-0  kutoka kwa  Azam na kuibua tetesi kuwa huenda katimuliwa.

Mwanza. Baada ya kupotea kwa muda kikosini,  kocha wa Alliance FC,Habibu Kondo ameibukia kwenye mazoezi ya timu hiyo leo Ijumaa ,huku akifafanua kilichokuwa kimemkimbiza katika timu hiyo.
Kondo ambaye aliajiriwa na timu hiyo kuchukua nafasu ya Athuman Bilali 'Billo' aliyetimuliwa, aliondoka ghafla kikosini baada ya mechi yao na Azam waliyofungwa mabao 5-0  Novemba 26  kwenye Uwanja wa Nyamagana Mwanza.
Baada ya kipigo  hicho,Kondo alipotea kwenye timu hiyo  huku mchezo uliofuata dhidi ya Yanga uliofanyika Novemba 29 wakilala mabao 2-1  na yeye akiwa hayupo benchi.
Leo wakati timu hiyo ikijifua katika Uwanja wa Nyamagana,kocha huyo wa zamani wa Mwadui FC,alionekana akiendesha mazoezi hayo sambamba na Kesy Mzirai.
Kondo amesema hakuwa na timu kutokana na mawasiliano hafifu baina yake na uongozi na kwamba kwa sasa amerudi rasmi kuendelea na majukumu yake.
"Baada ya ile mechi na Azam nilikuwa nimechoka nikaamua kuzima simu,lakini nilishiriki kuandaa programu kuelekea mechi ya Yanga,ila baadaye sikujua timu imeelekea wapi nikaona nitulie na juzi wakanitafuta wakaniambia tunaendelea na kazi ndio maana unaniona hapa".
"Mawasiliano yangu na uongozi hayakuwa mazuri,ila kazi inaendelea,nina mkataba wa miaka miwili Alliance japo sikutaka kueleza kilichotokea zaidi labda uwaulize viongozi kwa ufupi ni hivyo"amesema Kondo.
Kwa sasa Alliance inajiandaa na mchezo wake wa Kombe la Shirikisho(FA) dhidi ya , Transit Camp mechi itakayofanyika Desemba 21 katika uwanja wa Nyamagana.