Klopp hana presha kwa Mane, Mo Salah

Muktasari:

Tangu Liverpool ilipoanza kucheza soka la kiwango bora misimu michache ya karibuni, kila siku kumekuwa na uvumi wa kuhusu hatima ya washambuliaji hao wawili, Salah na Mane, kwamba wanasakwa na vigogo wengine na kwamba watanaswa waachane na maisha ya Anfield.

Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ana uhakika mkubwa kwamba atabaki na huduma za washambuliaji wake pacha matata kabisa, Mohamed Salah na Sadio Mane kwenye kikosi chake msimu ujao.

Tangu Liverpool ilipoanza kucheza soka la kiwango bora misimu michache ya karibuni, kila siku kumekuwa na uvumi wa kuhusu hatima ya washambuliaji hao wawili, Salah na Mane, kwamba wanasakwa na vigogo wengine na kwamba watanaswa waachane na maisha ya Anfield.

Hata hivyo, kocha Klopp hana shaka akiamini kwamba wachezaji wake hao hawataondoka.

Klabu zinazoripotiwa kuwataka ni pamoja na miamba ya Hispania, Barcelona na Real Madrid.

“Kuna klabu nyingi sana kubwa, lakini kama utakwenda Madrid au Barcelona, utashinda mataji ya ligi mara sita au saba ndani ya miaka 15.

“Bayern imeshinda mara tisa mfululizo na Juventus ni hivyo. Hayo ni mafanikio makubwa, lakini kitu kinachovutia ni kuwa na thamani kubwa mahali hapa.

“Tujaribu kufanya kila kitu kwenye klabu hii kumfanya kila mtu kujiona kuwa ni sehemu ya timu. Mpango ni kuwafanya wachezaji watakapoondoka, watazame nyuma na kuona siku muhimu kwenye maisha yao ya mpira ni wakati walipokuwa Liverpool.”