Klopp apewa ujanja kuhusu Bayern

Muktasari:

  • Silaha pekee anayotarajia kuitumia Klopp ni kuwapa kazi washambuliaji wake, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane kuhakikisha wanawashambulia Bayern Munich

Liverpool, England. Beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amewaambia hivi Liverpool wasitolee macho sana Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na badala yake wawe siriazi kwenye Ligi Kuu England kumaliza gundu.
Liverpool usiku wa leo, Jumanne itajimwaga huko Anfield kuikaribisha Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kocha Jurgen Klopp atakuwa kwenye presha kubwa jinsi ya kubalansi kikosi chake kutamba huko na kwenye Ligi Kuu England.
Lakini Neville amempa ujanja Klopp akimwambia asipambane vita nyingi na anachopaswa kukifanya kwa msimu huu ni kumalizia kila kilichopo kwenye mikono katika mchakamchaka wa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.
Liverpool kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, lakini ikiwa pointi sawa na vinara Manchester City lakini Liverpool ikiwa na mechi moja mkononi, ambapo kama itashinda itaweka pengo la pointi tatu.
Neville anamwambia Klopp asitumie nguvu sana huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuwachosha wachezaji jambo litakalomfanya ashindwe kotekote.
Klopp ataingia kwenye mechi hiyo ya leo huko Anfield akiwa hana huduma ya mabeki wake, Dejan Lovren, Joe Gomez na Virgil van Dijk kutokana na kuwa majeruhi na wengine kutumikia adhabu, hivyo kumfanya awe na chaguo la kumtumia Fabinho na Joel Matip kwenye beki ya kati.
Silaha pekee anayotarajia kuitumia Klopp ni kuwapa kazi washambuliaji wake, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane kuhakikisha wanawashambulia Bayern Munich mfululizo ili kuwafanya wasipande mbele kuja kusumbua mabeki wake.
Mchezo mwingine wa ligi hiyo ya kibabe Ulaya utakaopigwa leo, Olympique Lyon itakuwa nyumbani kuikaribisha Barcelona, wakati kesho Jumatano, Atletico Madrid ya Antoine Griezmann zitakuwa mwenyeji wa Juventus ya Cristiano Ronaldo, huku Pep Guardiola na chama lake la Man City atasafiri hadi Ujerumani kuwakabili FC Schalke 04.