Klopp anaona nyota tu ishu ya van Dijk

LIVERPOOL, ENGLAND. KOCHA wa Liverpool amesisitiza kwamba beki wa kati Virgil van Dijk anaendelea na matibabu na hakuna taarifa kamili juu ya lini anaweza kuwa sawa akiongeza kwamba majeraha yake hadi kupona yatachukua muda mrefu.

Beki huyo wa Liverpool alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Everton baada ya kukumbana na kipa wa timu hiyo Jordan Pickford wiki iliyopita na ripoti ambazo hazikuthibitishwa zilidai atakaa nje kwa miezi nane au saba.

Suala hilo linazidi kumuumiza kichwa kocha huyo kwa kuwa van Dijk kwake ni miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza ambaye uwepo wake ulikuwa unaifanya safu ya ulinzi ya Liverpool kuwa imara zaidi.

Licha ya nafasi yake kuchukuliwa na Fabinho ambaye alionyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Ajax ambapo ilishinda kwa bao 1-0, mambo yalionekana kuwa sio katika mchezo uliopita.

“Nafahamu kwamba mashabiki wengi wanapenda kumuona Virgil akiwa anacheza. Upasuaji utafanyika katika muda maalumu uliopangwa na wala hatuwezi kusema atacheza baada ya muda gani kwa kuwa watu wanatofautiana kwenye kupona,” alisema.

Fabinho ambaye anatumiwa kama mbadala wa beki huyo Mholanzi na kuonekana anaweza kulifanyia kazi vizuri eneo hilo, mchezo uliopita dhidi ya Sheffield United alionyesha kuwa na makosa mengi ikiwa pamoja na lile la kumchezea vibaya Oli McBurnie na kusababisha mwamuzi kuipa penalti Sheffield.

Lakini Klopp alimtetea na kusisitiza, refa wa mchezo huo hakuwa sahihi akiongeza kwake haikuwa penalti wala faulo.

“Ilikuwa ni katika harakati za kuuwania mpira. Kwenye mpira kuna vipindi tofauti. Unaweza kutotendewa haki kama hivi, lakini unatakiwa unyanyuke na usonge mbele,” alisema kocha huyo.