Klopp aiweka Liverpool patamu

Muktasari:

 

  • Liverpool imerejea kileleni katika Ligi Kuu England, baada ya kuichapa Fulham mabao 2-1.

London, England. Mkwaju wa penalti uliofungwa na James Milner umeirejesha Liverpool kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Engand.

Milner alifunga bao la penalti dakika ya 81 katika mchezo ambao Liverpool ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Fulham.

Liverpool imefikisha pointi 76 na kuwaacha wapinzani wao wakubwa Manchester City wakiwa na pointi 74 ikiwa pungufu mechi moja.

Liverpool ilitangulia kufunga dakika ya 26 kupitia kwa Sadio Mane kabla ya Milner kufunga. Bao la Fulham lilifungwa na Ryan Babel aliyewahi kucheza Liverpool.

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alisema kuwa ushindi dhidi ya Fulham umeiweka timu yake katika sehemu nzuri.

Klopp alisema ana amini Liverpool itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kupita miaka 29.

Alisema licha ya kukabiliana na upinzani kutoka Manchester City, lakini watapambana kupata mafanikio.

Liverpool inatarajiwa kuvaana na Tottenham Hotspurs katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Jumapili wiki hii.