Klopp aishiwi maneno kisa sare ya City

Muktasari:

Matokeo ya suluhu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Anfield dhidi ya Manchester City yamemtisha Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp, watapaswa kufanya kazi ya ziada ikiwa wanataka ubingwa.

Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amesema matokeo ya suluhu waliyoipata na Manchester City katika mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa Anfield jana, ilitokana na kubweteka kwa wachezaji wake.

Klopp alisema waliuanza mchezo huo vizuri wakitawala kila idara, lakini wachezaji wake wakajisahau na kuvimba vichwa kwa kuona wamewamiliki wapinzani wao.

Alisema hilo ndilo likawa kosa ambalo anashukuru kuambulia japo sare vinginevyo wangeadhirika wakiwa nyumbani.

"Kwa kweli ni masikitiko makubwa kuona kwamba tuliuanza mchezo vizuri tukitawala na kutengeneza nafasi vizuri, lakini baadaye wachezaji hawakuweza kulinda kiwango kile cha mwanzo na kutoa mwanya kwa City kujipanga.”

Klopp alisema walifanya kosa kubwa kutobaki na kiwango kile cha umiliki wa mpira kwa kipindi kirefu badala yake wakairuhusu City kuondoa hofu na kuanza kumiliki mpira jambo ambalo lilianza kuwatesa kadiri muda ulivyosonga.

Alisema baada ya kuanza kupoteana wachezaji walijikuta wakianza kuondoka mchezoni na kuacha kucheza soka lao badala yake kugeuka watafutaji wa mpira ambao sasa ulikuwa kwenye umiliki wa wapinzani wao.

Akiizungumzia penelti waliyopewa wapinzani wao dakika tano kabla ya mchezo kumalizika alisema ilikuwa halali na anashukuru kwamba walishindwa kuitumia kupata bao na wachezaji wake wanapaswa kujifunza kutokana na mchezo huo.

“Unapocheza na timu bora kama City unapaswa kulinda kiwango chako na kuumiliki mpira kwa muda wote ukifanya kosa la kuupoteza utataabika sana pale wao watakapoanza kuumiliki,” alisema.

Alisema baada ya mchezo huo kumalizika watapisha michuano ya mataifa kabla ya kurejea tena kujipanga kuendelea na ligi akiamini wanapaswa kuwa bora ili kuchuana na City na Chelsea katika mbio za ubingwa.

Timu hizo zote zina pointi 20 kwa michezo minane waliyocheza hadi sasa huku nyuma yao kukiwa na Arsenal na Tottenham zenye pointi 18 kila moja.