Klopp afyumu kisa Afcon

Muktasari:

Akizungumza katika kuelekea mchezo dhidi ya Manchester United utakaopigwa leo Jumapili, kocha huyo Mjerumani alisema uamuzi huo utawaathiri sana Liverpool kwa sababu imesajili wachezaji wengi mahiri wa Kiafrika.

LIVERPOOL, ENGLAND. KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amefyumu kisa Shirikisho la soka la Afrika (Caf) kuamua kubadilisha michuano ya Afcon 2021 ya huko Cameroon kuchezwa kuanzia Januari badala ya Juni.

Mwaka 2017, Caf ilipitisha mabadiliko ya michuano hiyo kufanyika kuanzia Juni badala ya Januari kwa sababu wengi wanakuwa na majukumu kwenye klabu zao huko Ulaya, lakini sasa kwa Afcon 2021 itarudishwa Januari jambo linalomvuruga Klopp.

Akizungumza katika kuelekea mchezo dhidi ya Manchester United utakaopigwa leo Jumapili, kocha huyo Mjerumani alisema uamuzi huo utawaathiri sana Liverpool kwa sababu imesajili wachezaji wengi mahiri wa Kiafrika.

“Kama tutafikia hatua ya kufanya uamuzi inapokuja suala la kusajili wachezaji, hilo litakuwa jambo kubwa zaidi. Unajua huwezi kuwa na wachezaji ambao wiki nne unazowahitaji zaidi wanakuwa hawapo kwenye timu yako. Ukweli hili jambo haliwasaidii wachezaji wa Kiafrika,” alisema Klopp.

“Nimekuwa nikitazama michuano ya Afrika na inavutia sana, lakini tatizo ni kwamba michuano yenyewe inafanyika katikati ya msimu. Lakini, ndio hivyo, hatuna uwezo. Kama tukisema hatuwaruhusu wachezaji, basi tunaadhibiwa.”

Kwenye michuano ya Afcon 2020, Klopp hatakuwa na huduma ya mastaa kama Mohamed Salah, Naby Keita na Sadio Mane ambao bila shaka watakwenda kuungana na timu zao za taifa kwenye mikikikimikiki hiyo.