Klopp: Tumepoteza umakini

London, England. Jurgen Klopp amekiri kuwa Liverpool imepoteza umakini baada ya mabingwa hao kuvurumishwa vibaya na Aston Villa kwa kupewa kipigo kizito cha kwanza baada ya miaka 57.

Aston Villa imekuwa timu ya kwanza tangu Tottenham ya 1963 kuifunga Liverpool mabao saba, wakati ilipoitandika mabao 7-2 kwenye Uwanja wa Villa Park, ikimaanisha kuwa kikosi cha Klopp kimekuwa cha mabingwa watetezi wa kwanza kuchakazwa kwa idadi hiyo tangu 1953, wakati kufungwa mabao mengi kwa mara ya mwisho.

Liverpool ilishindwa kuwa sawa tangu kipa Adrian kumzawadia Ollie Watkins kufunga bao la kuongoza.

Klopp alisema: “Kwa sababu tofauti, Aston Villa ilicheza vizuri, ilitulazimisha kufanya makosa. Bao la kwanza lilichangia, lakini haikutakiwa kuwa hivi.

“Tulishawahi kufungwa kama hivi, lakini haikuwa na mshituko huu, tumepoteza umakini. Kila Villa walipofanya shambulizi, tulishindwa kabisa kuwazuia. Vile ambavyo hutakiwi kufanya katika mchezo wa soka, sisi tulivifanya.”