Klabu ziwe makini timuatimua ya makocha

Muktasari:

Kuondolewa ghafla kwa makocha wakati wachezaji wameanza kuwazoea kunawavuruga kiufundi kwani wanapaswa kusahau yote waliyojifunza kwa kocha aliyetimuliwa na kuanza kujiandaa kumpokea kocha mpya.

UTAMADUNI wa klabu za soka nchini kuwatimua makocha waliowaajiri kwa mbwembwe unazidi kushika kasi. Kila msimu imekuwa ikishuhudiwa makocha wapya wakiajiriwa kisha ndani ya muda mfupi wakitupiwa virago wakati mwingine kukiwa hakuna sababu za maana.

Baadhi ya makocha wamekuwa wakitumuliwa kwa sababu eti zimeshindwa kucheza soka la kuvutia na sio kwa kukosa matokeo mazuri katika mechi zao za Ligi Kuu Bara, michuano ya Kombe la FA ama hata michezo za kimataifa. Wengine wamejikuta wakifungashiwa virago kwenye mechi za kirafiki za mabonanza, kuonyesha kuwa viongozi na wanachama wa klabu wana kasumba tu ya kuwafurusha makocha wao wanapojisikia.

Kama wadau wa michezo hususani soka, hatuoni kama ni kitu cha ajabu kwa klabu kuwaajiri makocha kisha kuachana nao iwe ndani ya muda mfupi ama mrefu. Ni kweli kabisa makocha huwa wanaajiriwa ili watimuliwe, lakini kwa upande mwingine hii fukuzafukuza hii ya makocha ni janga linalochangia kwa kiasi kikubwa kuzivuruga klabu husika na wachezaji kwa ujumla.

Makocha wamekuwa wakiajiriwa na kutemwa ndani ya vipindi vifupi wakiwa hata hawajatekeleza kwa ufanisi kazi zilizowaleta na pia kuzoeleka vyema kwa wachezaji wao. Kuondolewa ghafla kwa makocha wakati wachezaji wameanza kuwazoea kunawavuruga kiufundi kwani wanapaswa kusahau yote waliyojifunza kwa kocha aliyetimuliwa na kuanza kujiandaa kumpokea kocha mpya.

Kwa kawaida kila kocha huwa na mfumo na falsafa zake, hivyo pale wachezaji wanapobadilishwa kocha ndani ya muda mfupi huwachanganya na kuwavuruga sio kisaikolojia tu, bali hata kiufundi kwa vile hulazimika kuanza kuzoea falsafa na mfumo wa kocha mpya upyaa.

Hivyo wachezaji mara nyingi ndio wanaokuwa wahanga wakubwa wa badiliko ya makocha na kuzivuruga pia timu katika kupata mafanikio, hasa kama kocha anayekuja atakuwa mgumu kueleweka kwa haraka kwa wachezaji wake.

Kwa maana hiyo tulikuwa tunazikumbusha klabu kuwa, licha ya kwamba zimekuwa zikisaka mafanikio kupitia kwa makocha na hata wachezaji wanaowajiri kila msimu, lakini ni vyema wakajenga utamaduni wa kuwapa muda mrefu wa kuvinoa vikosi vyao kwa mafanikio ya timu.

Ni nadra kwa klabu za Tanzania kwa miaka ya sasa kuwapa mikataba ya muda mrefu makocha wao, kitu ambacho ni dhahiri viongozi wa wanachama wa klabu hizo ni kama hawaamini, kwani kwa uongozi bora wenye kuwaamini ni lazima wawape kandarasi ya muda mrefu. Kandarasi zinazotoa nafasi kwa makocha kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutekeleza mipango yao ya muda mfupi na ile mirefu na hata kama ikitokea wameshindwa kufikia malengo iwe rahisi kutimuliwa kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa ndani ya klabu kubwa duniani.

Ndio maana tumeamua kuzikumbusha klabu zote kuwa, zitimue makocha kila zinapojisikia, lakini ziwe na sababu na pia kumalizana nao kiungwana kwa mustakabali wa heshima la soka la Tanzania, ila wakijua kuwa wakati mwingine timuatimua hii inachangia kuwarudisha nyuma kimafanikio.