Klabu zisaidie kukuza vipaji vya soka la vijana kwa faida ya taifa

Muktasari:

Klabu zimekuwa zikifanya usajili kishabiki zaidi na kutafuta sifa, huku wakizidi kuonyesha namna gani zisivyothamini na kuwaamini vijana wanaowasajili ama kuwa nao kwenye vikosi vyao na kuendelea kuendeshwa na mhemko tu.

KWA wanaofuatilia soka la Tanzania, kwa muda mrefu wadau wa soka kuanzia viongozi wa FA ngazi za wilaya mpaka taifa na hata wale wa klabu na wanahabari wamekuwa wakiimba wimbo moja.

Wimbo wa kutaka kuwepo kwa uwekezaji katika soka la vijana kwa kuamini kuwa ndio msingi wa mafanikio ya kandanda letu. Ndio maana kila mara tumekuwa tukisikia zikitolewa maagizo kwa klabu kutoka FA juu ya kutakiwa kuwa na timu za vijana, huku ikianzishwa miradi na michuano mbalimbali ya vijana.

Bahati mbaya ni klabu chache zinazotekeleza jambo hilo kwa ufanisi, kiasi kwamba unaweza hata kuzihesabu. Hata kwenye madirisha ya usajili kumekuwa na ngonjera za klabu kusajili wachezaji vijana kwa nia ya kutaka kuwajengea misingi mizuri ya soka kwa manufaa ya taifa mbele ya safari.

Lakini ukifuatilia ni maigizo matupu katika mikakati na mipango hiyo inayotangazwa na sajili zinazofanywa na klabu. Turejee kwa sasa wakati madirisha madogo la usajili na hata yake makubwa, kumekuwa na mihemko ya kusajili wachezaji wa kina aina kutoka ndani na nje ya nchi, tena kwa fujo.

Klabu zimekuwa zikifanya usajili kishabiki zaidi na kutafuta sifa, huku wakizidi kuonyesha namna gani zisivyothamini na kuwaamini vijana wanaowasajili ama kuwa nao kwenye vikosi vyao na kuendelea kuendeshwa na mhemko tu. Klabu zimekuwa zikisajili wachezaji vijana kwa fujo, lakini wakishindwa kuwapa nafasi za kuzitumikia timu hizo, kitu kinachokatisha tamaa na kuua vipaji vyao. Klabu kubwa zimekuwa kama handaki la kuua vipaji vya vijana kwa kupenda kuwarundika pamoja na kushindwa kuwatumia kabla ya kuwaacha wakiwa wamechanganyikiwa.

Rejea kwenye mfano halisi wa mastraika Mohammed Rashid, Adam Salamba, Marcelo Keheza, Yohana Mkomola na wengine ndani ya klabu za Simba na Yanga uone ukweli wa jambo hili ulivyo. Wengi wa wachezaji hao vijana hawakupewa nafasi ya kucheza kwa vile kikosini kuna nyota wa kigeni na kusababisha wengine kutolewa kwa mkopo ama kutimka katika timu hizo.

Hili halijaanza leo ama jana ni jambo lililopo kwa muda mrefu na limekuwa likichangia kuua vipaji vilivyokuwa vikitarajiwa kuja kuwa msaada kwa taifa katika mechi za kimataifa. Mfano mdogo, kipa Manyika Peter Jr, alipokuwa Simba hakupewa nafasi akakimbilia Singida United na kung’ara kiasi cha kusajiliwa Kenya katika klabu ya KCB FC.

Azam ni moja ya klabu ya kutolewa mfano kwa kuthamini soka la vijana na kuwapa nafasi wachezaji wao, kwa mfano misimu kadhaa nyuma walikuwa na Mwadini Ali, lakini waliamua kumpa nafasi Aishi Manula aliyepo Simba kwa sasa.

Leo utazungumza nini kuhusu Manula, kipa huyo amekuwa mmoja ya makipa bora kabisa nchini kwa sasa akiwa tegemeo la timu yake na Taifa Stars. Yanga nao walivutiwa na kipa wa Serengeti Boys, Ramadhani Kabwili na kumsajili kikosini, lakini wamemtumia katika mechi ngapi? Kuna wachezaji wengine waliong’ara kwenye Kombe la Mapinduzi wakiwa na Yanga, leo wapo wapi?

Huku ni kuua vipaji vya wachezaji wetu vijana, ni sawa tu na alichokuwa anafanyiwa Jamal Mwambeleko na wengine waliosajili kwa mbwembwe na klabu hizo kubwa wakitokea timu za mikoani na kisha kukalishwa benchi na kuwa wachezaji wa benchini na jukwaani.

Kwa hali kama hii sio sawa na Mwanaspoti inakemea mtindo huu wa kuviza vipaji vya wachezaji unaofanywa na klabu kubwa. Wapo wachezaji wengine vijana ambao walikuwa waking’ara katika timu nyingine na kusajiliwa na klabu, kisha kuwenda kuzimika kabla ya kutolewa kwa mkopo.

Jambo la kushangaza ni kwamba klabu zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusajili wageni hata katika nafasi zisizohitaji nyota hao, hili linapaswa kubadilishwa. Wageni na wazoefu ni muhimu vikosini, lakini tuwaamini vijana tunaowasajili kwa manufaa ya taifa.

Pia klabu ziache kufanya usajili wa sifa na kutaka kufurahisha mashabiki, badala yake waangalie uhalisia wa soka letu na maendeleo yake. Ndio maana kila msimu wananyakua kila mchezaji aliyevuma msimu uliopita ama aliyewasumbua. Tusiwakatishe tamaa na kuua vipaji vyao kwani kufanya hivyo ni kulididimiza soka la Tanzania. Tunahaha kusaka timu kali ya taifa, kwa sasa hatuwajali na kmuwathamini vijana wetu.