Klabu zapoteza matumaini Ligi Kuu

Muktasari:

Kocha msaidizi wa Alliance, Kessy Mziray ambaye timu yake ni ya tatu kutoka mwisho alisema pamoja na kuwapigia simu wachezaji wake kujua maendeleo yao wakati huu, bado haisaidii.

Dar es Salaam. Makocha wanaopigania kubaki ligi kuu wameonyesha wasiwasi wa kutibuliwa mipango yao na kueleza namna wanavyopata changamoto ya kuwasimamia wachezaji kipindi hiki wanachofanya mazoezi binafsi kwa ajili ya tahadhari ya ugonjwa wa corona.

Timu za Singida United ambayo ni ya mwisho kwenye msimamo ikiwa na pointi 15, Mbao (22), Alliance (29), Mbeya City (30), Ndanda (31) na KMC, Mtibwa Sugar na Lipuli kila moja ina pointi 33 zinapambana kujinasua katika dhahama ya kushuka daraja ligi itakapoendelea.

Makocha wa timu hizo wameonyesha kukata tamaa ya wachezaji wao kurudi katika ubora uleule ligi itakapoendelea baada ya janga la corona kupita huku wasiwasi wa kutengeneza majeruhi wengi ukitanda.

Makocha hao kwa nyakati tofauti jana walisema wanapata changamoto kubwa kufuatilia mazoezi ya wachezaji wao, kipindi hiki ambacho wanajifua katika mazoezi binafsi.

Kocha msaidizi wa Alliance, Kessy Mziray ambaye timu yake ni ya tatu kutoka mwisho alisema pamoja na kuwapigia simu wachezaji wake kujua maendeleo yao wakati huu, bado haisaidii.

“Mnapofanya mazoezi ya pamoja kuna kasoro kama kocha unazirekebisha na kutengeneza ubora, kipindi hiki ni kama wako mapumziko, watakaporejea unaanza moja.

“Na wachezaji wenyewe wengi wao sidhani kama wanafanya, na hata wanaofanya sio rahisi kufanya kwa muda na kiwango, sijui ligi itakapoendelea itakuwaje, hii ni changamoto sana,” alisema.

Kocha wa Singida United, Ramadhan Nswanzurwimo alisema hakuna njia mbadala ya kufuatilia mazoezi ya wachezaji wake zaidi ya kuwapigia simu, “kila unayemuuliza kama anatekeleza progoramu aliyopewa anajibu ndiyo, naombea iwe hivyo, japo nayo siyo garantii kwamba watarejea kwa kiwango kizuri, naumiza kichwa kujua vipi tutaimarika na kuwa sawa ligi itapoendelea.”

Kocha wa Mbeya City, Amri Said alisema wachezaji wanapaswa kutambua mpira ni kazi inayowaingizia kipato, klabu pia inamtegemea kwa mafanikio na familia yake inamtegemea aihudumie kwa kazi hiyo, hivyo wasibweteke.

Kocha wa Mbao, Abdul Mutiki alisema wanapata wakati mgumu kuwafuatiliwa wacheza na kwamba anaomba janga la corona lipite waanze mazoezi ya pamoja kuhakikisha wanajinasua mkiani.