Klabu za England zinavyopiga pesa udhamini wa jezi

Muktasari:

Wadhamini 10 kati ya 20 waliopo kwenye timu za Ligi Kuu England msimu huu ni makampuni ya kamari. Kiongozi msaidizi wa chama cha Labour, Tom Watson amedai kwamba atazizuia timu kusaini dili za udhamini na makampuni ya kamari huku baadaye, kama chama chake kitaingia madarakani.

LONDON, ENGLAND. WADHAMINI wa Manchester United kwenye jezi zao, Chevrolet bado wanashika namba moja kwa kutoa mkwanja mrefu kwenye Ligi Kuu England kwa mujibu wa mwandishi wa habari Alex Miller.

Dili hilo la udhamini waliloingia Man United na kampuni hiyo ya watengeneza magari mwaka 2012, linatajwa kuwa na thamani ya Pauni 64 milioni kwa mwaka. Hiyo ina maana kwamba Man United inavuna Pauni 64 milioni kila mwaka kutokana na jina la Chevrolet kutokea kwenye jezi zao. Wadhamini wa kwenye jezi za Brighton, American Express ndio wanaolipa pesa kidogo zaidi kuliko wote kwenye Ligi Kuu England, Pauni 1.5 milioni kwa mwaka. Lakini, wadhamini hao wapo kwenye ubia pia na Seagulls, ambao pia wanamiliki haki ya jina la uwanja wa nyumbani wa timu hiyo.

Lakini, kwenye mgao huo wa pesa za wadhamini kwenye jezi umeonyesha wazi tofauti iliyopo baina ya klabu za Big Six na nyingine. Kwa mfano tu, dili la West Ham United na Betway linashika namba saba kwa ukubwa, lakini ni kama asilimia 28.6 ya mkwanja wanaovuta Tottenham Hotspur kupitia wadhamini wao AIA ambao wapo kwenye namba sita.

Wadhamini 10 kati ya 20 waliopo kwenye timu za Ligi Kuu England msimu huu ni makampuni ya kamari. Kiongozi msaidizi wa chama cha Labour, Tom Watson amedai kwamba atazizuia timu kusaini dili za udhamini na makampuni ya kamari huku baadaye, kama chama chake kitaingia madarakani.

Lakini, wadhamini wanaotamba kwenye Ligi Kuu England wengi ni makampuni ya kutoka Asia huku shughuli zake nyingi zikifanyika nje ya Uingereza. Hii hapa orodha ya wadhamini wa kuu wa kwenye jezi za Ligi Kuu England na mkwanja wao wanaotoa kwa mwaka.

Man United wanavuna Pauni 64 milioni kupitia Chevrolet, wakati mahasimu wao Manchester City wanavuna Pauni 45 milioni kupitia udhamini wa Etihad, huku Arsenal wakishika namba tatu kwa kuingiza Pauni 40 milioni kupitia Fly Emirates, kiwango sawa wanacholipwa Chelsea kupitia Yokohama na Liverpool kupitia Standard Chartered. Chelsea na Liverpool kila moja zinavuna Pauni 40 milioni kwa mwaka kupitia wadhamini wao wakuu kwenye jezi. Sita bora inakamilishwa na Spurs, ambao wanavuna Pauni 35 milioni kupitia AIA.

West Ham wao wanavuna Pauni 10 milioni kupitia Betway, huku Everton wakishika namba nane wakivuna Pauni 9.6 milioni kupitia SportPesa, huku Wolves wanavuna Pauni 8 milioni kupitia ManBetX na Southampton wanakamilisha 10 bora wakivuna Pauni 7.5 milioni kupitia wadhamini wao LD Sports. Burnley wanavuna Pauni 7.5 milioni kupitia wadhamini wao LoveBet, wakifuatiwa na Crystal Palace wakivuna Pauni 6.5 milioni kupitia wadhamini wao ManBetX, sawa na kiwango wanachovuna Newcastle United kupitia Fun88 na Watford wakibuna kupitia Sportsbet.io.

Aston Villa wanavuna Pauni 6 milioni kupitia W88, wakati Bournemouth wanaweka mfukoni Pauni 5 milioni kwa udhamini wa M88, huku Leicester City wanaingiza Pauni 4 milioni kwa udhamini wa King Power, Sheffield United Pauni 3.5 milioni kupitia USG, Norwich City Pauni 3 milioni kupitia Dafabet na Brighton wakiweka kibindoni Pauni 1.5 milioni kupitia wadhamini wao wakuu kwenye jezi American Express.