Klabu Ligi Kuu kumrudisha Djuma Tanzania

Muktasari:

Kocha Masoud Djuma amesema anaondoka nchini, lakini atarejea Tanzania iwe kutembea au kufundisha soka.

Klabu ya Simba ilivunja mkataba na kocha huyo raia wa Burundi, baada ya kudaiwa kushindwa kuelewana na Kocha Mkuu Patrick Aussems.

Dar es Salaam. Licha ya kumalizana na Simba, Masoud Djuma amesema anakwenda Burundi kupumzika, lakini atarudi Tanzania muda siyo mrefu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema hana tena mkataba na Simba baada ya pande zote mbili kufikia mwafaka.

Djuma aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, alisema ana mpango wa kurudi kufanya kazi Tanzania baada ya kuishi vyema na Watanzania katika muda wote aliodumu nchini.

"Nitarudi Tanzania haijalishi kuwatembelea mashabiki wangu walioniunga mkono nikiwa Simba au kwenye kazi nyingine, lakini nitarudi siku siyo nyingi ngoja nikapumzike  kwa muda nyumbani (Burundi)," alisema kocha huyo.

Akizungumzia kulipwa stahiki zake Simba, Djuma alisema  ‘mambo’ yamekwenda vyema na anarejea Burundi akiwa roho kwatu baada ya kumalizana na vigogo wa Simba.

Hata hivyo, Djuma aliyekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba, aligoma kuzungumzia madai ya kutokuwa na uhusiano mzuri na Kocha Mkuu Patrick Aussems sanjari na klabu zinazomnyemelea.

Habari za ndani zimedai Djuma amefanya mazungumzo na baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ili kumpa mkataba baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

Klabu zinazohusishwa kumtaka mshambuliaji huyo nyota wa zamani wa kimataifa wa Burundi ni Yanga, Coastal Union, African Lyon.